CHAMA cha wandishi wa habari
wanawake Tanzania (TAMWA) kimebaini kuwa kuongezeka kwa kesi za ukatili
wa kijinsia kumechangiwa na kutojua sheria na kutokuwepo kwa mifumo
madhubuti ya kuripoti ikiwa ni pamoja na jamii kutobadilishana mawazo.
Akiwasilisha ripoti
ya utafiti huo Dar es salaam jana Mkurugenzi Mtendaji wa Tamwa, Valerie
Msoka alisema hayo yamebainika wakati wa utafiti wa awali uliofanywa na
mashirika ya kutetea haki za binadamu ambayo ni Chama cha wanasheria
wanawake (TAWLA), Chama cha wanasheria wanawake Zanzibar(ZAFELA), Kituo
cha usuluhishi (CRC), Mtandao wa jinsia Tanzania (TGNP) pamoja na Tamwa
bara na Zanzibar.
Alisema kuwa utafiti huo umebaini
kuwa asilimia 17 tu ya wananchi ndiyo wenyeuelewa wa sheria za ukatili
hali inayochangia jamii kutofatilia haki zake pindi zinapovunjwa ambapo
na wakati mwingine kutokuripoti kabisa kesi hizo.
“Tumebaini kuwa Lindi vijijini
ndiyo inayoongoza kwa kuwa na uelewa mdogo wa asilimia 12 ya wakazi
ukilinganisha na asilimia 21 ya uelewa kwa Wilaya zote kwa mfano Ofisa
wa Polisi wa Wilaya ya Lindi alisema kesi nyingi huripotiwa katika hatua
ya familia na hufikishwa mahakamani baada ya kushindwa kupata suluhu na
hivyo kuwa katika hatari ya kupata haki” alisema Msoka.
Alibainisha kuwa hali ya kutokuwa
na mfumo maalum wa kuripoti kunaweka mazingira ya kutokupatikana kwa
haki ikiwa ni pamoja na kukosekana kwa takwimu sahihi ya kesi za
ukatili.
Msoka alizitaja Wilaya
zilizohusika katika utafiti huo kuwa ni Wete(Pemba kaskazini), Magharibi
(Unguja), Kusini Unguja(Kusini Unguja), Kisalawe (Pwani) Newala
(Mtwala), Lindi vijijini(Lindi), Mvomero (Morogoro) na Wilaya za
Kinondoni na Ilala, Dar es Salaam.
Alisema kwa pamoja mashirika hayo
yatatekeleza mpango wa usawa wa Jinsia na Uwezeshaji wa Wanawake(GAWE)
ambao unafanywa kwa ushirikiano na Serikali ya Denmark.
No comments:
Post a Comment