Tuesday, February 26, 2013

KWA NEEMA FM NA RADIO IMANI ZAFUNGIWA...CLOUDS YATOZWA FAINI

 
Picture
Makamu Mwenyekiti wa Kamati Maadili ya Utangazaji nchini, Walter Bgoya (katikati) akizungumza na wanahabari leo jijini Dar es Salaam ukumbi wa habari Maelezo (picha: TheHabari.com)
Picture
Waandishi wa habari wakiwa katika mkutano huo (picha: TheHabari.com)
Mamlaka ya Mawasiliano nchini Tanzania, TCRA, imetoa adhabu ya kufungia na kulipa faini vyombo vya habari vitatu vya Clouds Radio FM (Dar es Salaam), Kwa Neema Radio FM (Mwanza) na Imani Radio FM (Morogoro) kutokana na sababu za kurusha matangazo yanayokwenda kinyume na sheria za Mamlaka hayo.

Katika adhabu hiyo, Clouds FM Radio  imepewa onyo kali la kutokurudia kosa linaloenda kinyume cha sheria za TCRA, pia imeamriwa kulipa faini ya Shilingi milioni 5  ndani ya kipindi cha mwezi mmoja kuanzia leo siku ya kutolewa agizo. Hii ni kutokana na kipindi chake cha Power Breakfast na pia kwa kuendesha kipengele cha “Jicho la Ng’ombe” kisicho na maadili. Vile vile redio hiyo imeamriwa kutokuanzisha kipindi kinachofanana na “Jicho la Ng’ombe”.

Aidha, Kwa Neema Radio FM na Imani Radio FM zimefungiwa kwa muda wa miezi sita.

Kwa Neema imefungiwa kutokana na kuhamasisha kukuza mgogoro uliozuka hivi karibuni mkoani Geita wa nani mwenye haki ya kuchinja ng’ombe kati ya Waislam na Wakristo wakati Imani Radio FM imefungikwa kwa kosa la kuhamasisha watu kususia na kutoshiriki kwenye agizo la Serikali la hesabu ya watu na makazi, Sensa, 2012.

Adhabu hizo zimetokana na maamuzi ya Kamati ya Maadili ya Utangazaji nchini kama ilivyoelezwa mbele ya waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam na Makamu Mwenyekiti wa Kamati hiyo, ndugu Walter Bgoya.

Hata hivyo, Kamati ya Maadili imeweka mlango wazi kwa vituo hivyo kukata rufaa endapo havitaridhika na adhabu vilivyopewa kutokana na makosa vilivyodaiwa kuyafanya.

Kamati hiyo imevitaka vyombo vyote vya habari kufanya kazi kwa kuzingatia Kanuni Sheria na maadili ya tasnia hiyo ili kuepuka kuzua migogoro kwa wananchi ambao wamekuwa wakiviamini.
Picture
(picha: TheHabari.com)
Picture
Gari la Kituo cha Imani FM kilichofungiwa likiwa Idara ya Habari Maelezo leo (picha: TheHabari.com)

No comments:

Post a Comment