Monday, January 7, 2013

ASKARI WAWILI WAUAWA NA WANANCHI KISA MENO YA TEMBO HUKO KARAGWE

ASKARI Polisi wawili wa kituo Kidogo cha Polisi, BENACCO wilayani Ngara mkoani Kagera wameuawa na wananchi baada ya kushambuliwa kwa silaha za jadi huku gari walilokuwa nalo likichomwa moto katika kijiji cha Kasheshe, kata ya Rugu Chanyamisa wilayani Karagwe mkoani Kagera kwa tuhuma za kujihusisha na wizi wa meno saba ya tembo yenye kukadiriwa kuwa na uzito wa kilogramu 34.

Mkuu wa Jeshi la Polisi Inspekta Said Mwema amesema askari waliouawa wametambulika kuwa ni Sajenti Thomas Magiro namba E1445 na Koplo Damas Kisheke namba E8889 wa kituo kidogo cha Polisi BENACCO wilayani Ngara.

Askari mwingine ambaye amejulikana kwa jina moja la Brighton, aliwatoroka wananchi hao na kujisalimisha katika kituo cha polisi cha Kyanyamisa, akiwa na silaha yake.

Imeelezwa kuwa, baada ya jeshi la polisi kupata habari za kuwepo kwa biashara ya meno hayo, askari watatu wakiwa na gari aina ya Noah (namba hazijatambulika kutokana na gari hilo kuchomwa moto na kuteketea) waliondoka wakiambatana na wafanyabishara wawili, Shabani Abubakary na Gerald wote wa BENACCO, ili wajidai kuwa wanunuzi wa meno hayo yaliyokuwa yakiunzwa na Raymond na mwenziye.

Walipokaribia wilayani Karagwe, wafanyabiashara hao walitangulizwa nyumbani kwa mwuzaji, Raymond ili kuzungumza naye wakijifanya walitaka kununua meno ya tembo. Baada ya wanunuzi hao kuonyeshwa shehena ya meno hayo, waliwapigia simu askari waliokuwa wameambatana nao. Askari wale walipofika waliyafunga meno hayo kwenye gunia, na ndipo wanunuzi wakawageuka wauzaji.

Baada ya wauzaji kuona hivyo, walikimbia lakini baadaye waligundua kuwa walichezewa dili na askari, ndipo nao walipoamua kuwapigia simu wananchi wakiwaeleza kuwa wameibiwa na majambazi huku wakiwatajia aina ya gari ya majambazi na rangi yake.

Baada ya askari hao kuanza kuondoka kurudi BENACCO wakiwa na shehena hiyo ya meno ya tembo, walipofika eneo hilo walikuta njia imefungwa kwa mawe na huku kukiwa na kundi kubwa la wananchi wenye silaha za asili na ndipo askari hao walipojitokeza na kujitambulisha kwa wananchi, lakini walishambuliwa na kuuawa papo hapo.

Hili ni tukio la pili askari kuuawa na wananchi ambapo katika tukio la kwanza lililotokea Desemba 15 mwaka jana askari wengine wawili  Koplo Pascal na Konstebo Alex wa Kikosi cha Usalama Barabarani wilayani Ngara waliuawa kwa kushambuliwa na wananchi wakati ambapo walikuwa wamekwenda katika kijiji cha Mugoma kwa lengo la kukagua pikipiki mbovu na zisizokuwa na usajili.

Mganga mfawidhi wa hospitali teule ya Nyakahanga wilaya ya Karagwe Dkt. Andrew Cesari amethibitisha kupokea miili ya marehemu hao na alisema kuwa uchunguzi wa kitabibu umebainisha kuwa vifo vya marehemu hao vilitokana na kipigo kikali kilichosababisha majeraha ya kuvuja damu nyingi na kupelekea mauti hayo.

Kamanda wa jeshi la polisi mkoa wa Kagera Philipo Kalangi amefika katika eneo la tukio na kuthibitisha kuwa waliouwawa ni askari amesema kuwa uchunguzi unaendelea wa kubaini shughuli ilikuwa imewaleta askari hao na chanzo cha vifo vyao, pia amewataka wananchi kutojichukulia sheria mikononi.

---
taarifa via blogu za: KajunaSon na KatulandaNews

No comments:

Post a Comment