Friday, December 28, 2012

WAZAZI WENZA, MWASITI, MAUA WAZUIA BWANA HARUSI KUFUNGA NDOA


 
Habari imeandikwa na Peti Siyame, Habari Leo, Sumbawanga

WAKATI Wakristo wakiungana kusherehekea Sikukuu ya Krismasi usiku wa Desemba 24, Bwana harusi, Crispin Saadani (34) aliyekuwa akisherehekea siku hiyo kwa kufunga ndoa na mchumba wake, alijikuta akizuiwa kuweka ahadi hiyo ya maisha baada ya wanawake wawili alioishi na kuzaa nao, kuingilia kati.


Akiwa ndani ya jengo la Kanisa Katoliki, Jimbo la Sumbawanga, Parokia ya Familia Takatifu na mchumba wake aliyetambulika kwa jina moja la Elizabeth, bwana harusi huyo mtarajiwa alijikuta akizuiwa kupanda madhabahuni na wanawake wawili waliojitokeza huku wakijitambulisha kuwa ni wake zake.


Wakati Padri Boniface Nyama akijiandaa kufunga ndoa hiyo, wanawake hao, Maua Chatakwa na Mwasiti Mbegele (27) walifika kanisani hapo na kumuita mmoja wa wa wazee wa kanisa hilo.


Kisa chenyewe


Akisimulia kisa hicho, Mzee huyo wa Kanisa ambaye hakutaka kutajwa jina lake gazetini, alisema Crispin na mchumba wake, siku hiyo saa sita usiku katika mkesha wa Krismasi walikuwa miongoni mwa maharusi watarajiwa 32 waliokuwa wameketi katika benchi wakisubiri zamu zao ili wapande madhabahuni kufungishwa ndoa na Padri Nyama.


Alisema Mwasiti na Maua walitinga kanisani humo, wakamwita na kumweleza kuwa wamemfuata bwana wao ambaye wamesikia anafunga ndoa na mwanamke mwingine huku wakitoa ishara za kumwonesha.


Mwasiti ambaye ni mkazi wa Bangwe mjini hapa anayejishughulisha na ufundi wa kushona nguo za kike, alidai kuishi kinyumba na Crispin na kuzaa naye mtoto aitwaye Henry mwenye umri wa mwaka na nusu. Naye Maua, mkazi wa Jangwani mjini hapa, alidai aliishi kinyumba na Crispin na kuzaa naye watoto wawili.


Akisimulia hali ilivyokuwa, Mwasiti alidai aliishi kinyumba na mume huyo na kuzaa naye mtoto wa kiume, Henry, lakini walitengana baada ya kubaini kuwa mumewe alikuwa na wanawake wengine wawili zaidi ambao ni Maua na Elizabeth.


“Nilipomtaka aachane nao alikataa na kusema kuwa ataishi nao kama wake zake. Alianza kutupangia zamu, lakini nilishindwa pale alipoenda kulala kwa Maua siku tatu ya nne nilikusanya nguo zake na kupeleka huko, ukawa mwisho wetu, ” alidai Mwasiti na kuongeza kuwa kisa hicho kilitokea mwaka huu.


Mwasiti alikiri aliposikia Crispin anataka kumuoa Elizabeth, alimshawishi Maua wakamwekee kizuizi ili tu asifunge ndoa na Elizabeth ndipo walipokodi teksi iliyowafikisha kanisani hapo saa tano usiku.


Kwa mujibu wa Mwasiti baada ya kueleza mkasa huo kwa Mzee wa Kanisa, walikaribishwa katika moja ya chumba kanisani hapo na kukutana na baadhi ya mapadre na wazee wa Kanisa na makatekista.


Alidai baada ya mjadala mrefu ilikubaliwa kuwa shauri hilo lifikishwe siku inayofuata kwa Paroko wa Kanisa hilo, Padri Leonard Teza, ambaye pia ni Mwanasheria wa Jimbo.


Mzee huyo alikiri kumfuata Crispin ambaye ni mkazi wa Utengule katika Manispaa ya Sumbawanga, alipoketi na mchumba wake akisubiri kupanda madhabahuni na kumuomba atoke nje ya Kanisa kwa dharura na wakaishia kuahirisha ndoa hiyo.


Mwasiti ambaye alikuwa muwazi kwa gazeti hili, alidai Crispin aliitwa na kukiri kuwa anawafahamu na amezaa nao huku wao wakisisitiza kuwa wapo tayari afunge ndoa lakini awaeleze jinsi atakavyowatunza watoto hao watatu.


Ahadi ya matunzo


“Crispin alikubali kutupatia mtaji wa Sh 100,000 kila mmoja wetu huku mimi akidai atanipatia fedha hizi za mtaji Aprili 25, mwaka kesho na mwenzagu Maua aliahidiwa kupewa kiasi hicho cha fedha.“Pia aliahidi kutoa Sh 240,000 na seti ya TV ya inchi 9 aliyochukua kwake (Mwasiti) ifikapo Machi mwaka huu,” alisema Mwasiti.


Wazazi waja juu


Kwa mujibu wa madai ya baadhi ya mashuhuda, wazazi wa bibi harusi walisema ndoa hiyo isifungwe tena kwa kuwa bwana harusi amewafedhehesha huku baadhi ya wakazi wa mjini hapa wakimtuhumu bwana harusi kwa kusababisha hayo yote.


“Kosa hapa wa kulaumiwa ni huyu bwana harusi, kwa nini asiwafahamishe wale wake zake wengine kuwa anatarajia kufunga ndoa?” Alihoji mmoja wa mashuhuda.


Akizungumza kwa njia ya simu jana, Padri Teza alikiri kutokea kwa mkasa huo, lakini hatimaye alisema baada ya kukutana na wanawake hao walifikia makubaliano na hatimaye ndoa hiyo ilifungwa Jumatano asubuhi.


No comments:

Post a Comment