Waziri
wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo Dk. Fenella Mukangara
(kushoto) akipokea taarifa ya SACCOS ya Ibwera iliyopo wilayani Bukoba
kutoka kwa Benedicta Peter ambaye ni katibu msaidizi. SACCOS hiyo
ilipata mkopo wa shilingi milioni tano kutoka mfuko wa maendeleo ya
vijana na kuvikopesha vikundi mbalimbali vya maendeleo vya vijana.
……………………………………………………….
Na Anna Nkinda – Maelezo, Kagera
Serikali imeombwa kuongeza kiasi
cha mkopo kinachotoa kwa vijana kupitia mfuko wa maendeleo wa vijana na
Halmashauri za wilaya kwani kiwango kinachotolewa kwa sasa cha shilingi
milioni tano kwa vyama vya Kuweka Akiba na Kukopa (SACCOS) ni kidogo
ukilinganisha na mahitaji ya mkopo huo.
Ombi hilo limetolewa jana na
baadhi ya vijana waliopata mkopo huo kupitia SACCOS ya Ibwera na
halmashauri ya wilaya ya Bukoba wakati wakiongea kwa nyakati tofauti na
Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo Dk. Fenella Mukangara
alipotembelea wilaya hiyo ili kuona jinsi fedha hizo zilivyoweza
kuwasaidia vijana kujikwamua kiuchumi.
Vijana hao walisema kuwa fedha za
mkopo walizozipata zimewasaidia kujiinua kiuchumi ikiwa ni pamoja na
kuajiri vijana wenzao, kupanua mitaji ya biashara zao, kulipa karo za
shule za watoto wao na kujikwamua kimaisha tofauti na ilvyokuwa awali
kaba hawajapata mkopo na kufanya shughuli za ujasiriamali.
Kwa upande wake mkazi wa kijiji
cha Ibwera Ibrahim Mulokozi ambaye alipata mkopo wa shilingi laki nne
kupitia SACCOS ya kijiji hicho alisema kuwa ameweza kununua matandazo na
kulipa wasaidizi wanaohudumia shamba lake la migimba na kahawa
ambalo ni la mfano kwa vijana na wazee wanaotoka kata ya Ibwera, Mikoni
na Nyakibimbili na kwenda kujifunza na kuchukua miche ya migomba.
Alisema kuwa anakabiliwa na
changamoto za kutokuwa na fedha za kuendeleza shughuli za kilimo, kutoka
na mbolea ya kutosha ya kurutubisha shamba, bei ya miche ya kahawa
kupanda kutoka shilingi 50 hadi 500 kwa mche mmoja, kuendelea kutumia
jembe la mkono, kutokuwa na masoko ya uhakika hasa soko la ndizi na
magonjwa ya migomba.
Naye katibu wa kikundi cha
Msifuni Johanes Joel ambacho kilipata mkopo wa shilingi milioni moja na
laki tano kutoka Halmashauri ya wilaya ya Bukoba alisema kuwa kikundi
chao kinajishughulisha na kazi ya ukulima wa samaki na walianza na
bwawa moja na hivi sasa wana mabwawa matatu na wanampango wa kuhakikisha
kuwa kila mwanakikundi anakuwa na bwawa lake.
“Changamoto zinazotukabili ni
kutokuwa na mtaji wa kutosha, wanachama kutokuwa na elimu ya kuendesha
na kusimamia au kutunza miradi na kufanyiwa hujuma kwa mradi wetu wa
samaki ikiwa ni pamoja na kuibiwa na kuharibiwa kwa mabwawa hasa
nyakati za usiku na watu wasiopenda kufanya kazi za maendeleo”, allisema
Joel.
Kwa upande wake waziri Dk.
Mukangara aliwataka vijana wa kijiji hicho kufanya kazi kwa kujituma na
kujiunga katika vikundi vya maendeleo jambo ambalo litawafanya waweze
kupata mikopo kutoka mfuko wa maendeleo ya vijana na halmashauri ya
wilaya na hivyo kuweza kujishughulisha na kazi za upandaji wa miti,
kilimo cha samaki na ufugaji wa ng’ombe wa maziwa na nyuki.
Dk. Mukangara alisema, “Vijana ni
lazima mfanye kazi na kuachana na tabia ya uvivu, kufanya kazi si
lazima uajiriwe bali unaweza kujiajiri wewe mwenyewe kama hapa Ibwera
kunahali ya hewa nzuri na milima mingi haina miti mnaweza kuwa na mradi
wa kupanda miti na kufuga nyuki ambao watawapatia asali na mkiiuza
mtapata fedha nahivyo kujikwamua kiuchumi”.
Kwa upande wa mafunzo ya
ujasiriamali waziri Dk. Mukangara alisema kuwa wizara yake inavituo vya
kuwajenge uwezo vijana hivyo basi kama wahusika ambao ni vijana watakuwa
tayari kupata mafunzo ya ushirika na mafunzo mengine kama ya uongozi,
stadi za maisha watayapata na yatawasaidia katika maisha yao.
Waziri Dk. Mukangara alikuwa
mkoani Kagera kwa ajili ya kukagua SACCOS na vikundi vya vijana
vilivyopata mkopo kutoka mfuko wa maendeleo ya vijana ili kuona fedha
hizo zimewasaidiaje vijana kujikwamua kiuchumi. Katika wilaya ya Bukoba
alilitembelea shamba la mfano la kahawa na migomba, kikundi cha
burudani cha Rugazi na shamba la samaki la kikundi cha Msifuni.
No comments:
Post a Comment