Sunday, December 30, 2012

IBF YAMTANGAZA LUCAS RUTAINURWA WA KITWE GENERAL TRADERS KAMA PROMOTA WA MWAKA 2012

Branco Milenkovik wa kampuni ya  Branco Sports Productions  ya Johannesburg Afrika Kusini aliyeteuliwa na IBF kwa mwaka 2012,
…………………………………………………………….

Shirikisho la Ngumi la Kimataifa (IBF) katika bara la Afrika, Ghuba ya Uajemi na Mashariki ya Kati limemtamngaza bwana Lucas Rutainurwa wa kampuni ya Kitwe General Traders ya jijini Dar-Es-Salam kama Promota wa mwaka 2012.
 Akitangaza habari hizi, Rais wa IBF katika bara la Afrika, Ghuba ya Uajemi na Mashariki ya Kati Mtanzania Onesmo Ngowi alisema kuwa bwana Lucas Rutainurwa alifanikisha Watanzania wawili kuwa mabingwa wa IBF katika bara la Afrika, Ghuba ya Uajemi an Mashariki ya Kati mwaka unaoishia Desemba 2012.
 Katika harakati zake za kuipa Tanzania sura ya kimataifa katika tasnia ya ngumi za kulipwa Rutainurwa na kampuni yake ya Kitwe General Traders waliandaa mapambano makubwa mawili ambayo yalizidi maandalizi ya mapambano yote yaliyowahi kufanyika Tanzania kwa miaka ya karibuni.
 Mwezi April mwaka 2012, Rutainurwa na Kitwe General Traders waliandaa pambano lililowakutanisha mabondia Francis Cheka na Mada Maugo wote wa Tanzania kugombea mkanda wa IBF bara la Afrika, Ghuba ya Uajemi na Mashariki ya Kati katika ukumbi wa PTA jijini Dar-Es-Salaam. Katika mpambano huo bondia Francis Cheka aliibuka kidedea baada ya kumsimamisha Maugo katika raundi ya nane.
 Francis Cheka alitetea vyema mkanda wake huo tarehe 26 Desemba jijini Arusha alishinda kwwa points bondia Chimwemwe Chiotcha kutoka nchini Malawi katika pambano lao la raundi 12.
 Mwezi wa nane mwaka 2012, Rutainurwa na Kitwe General Traders waliandaa mpambano mwingine kati ya bondia Ramadhani Shauri wa Tanzania na Sunday Kizito kutoka Uganda kugombea mkanda wa IBF katika bara la Afrika, Ghuba ya Uajemi na Mashariki ya Kati katika uzito wa Unyoya (Featherweight).
 Katika mpambano huo bondia Ramadhani Shauri wa Tanzania alimsimamisha Sunday Kizito kutoka Uganda katika raundi ya 9 na kutangazwa kuwa bingwa mpya wa IBF.
 Kupatikana kwa mabingwa hao, kumeifanya Tanzania kuwa nyumbani kwa mabingwa wawili wa IBF na hivyo kuiweka nchi hii katika ngazi moja na chache duniani hususa katika bara la Afrika zikiwemo Afrika ya Kusini, Ghana, Morocco, Algeria na Cameron.
 Shirikisho la Ngumi la Kimataifa lina makao yake makuu yanayoratibu bara la Afrika, Ghuba ya Uajemi na Mashariki ya Kati kutokea katika jiji la Dar-Es-Salaam, Tanzania. Hii ni heshima ya kipekee kwa nchi ya Tanzania kwani nchi nyingi zinagombania kuwa makao makuu ya shirikisho hii kubwa kuliko yote duniani.
 IBF imemshukuru sana bwana Lucas Rutainurwa na kampuni yake ya Kitwe General Traders kwa mafanikio haya mazuri.
 Bwana Lucas atapewa tuzo
yake la kuwa promota wa mwaka wa IBF katika bara la Afrika mwaka 2012 rasmi wakati wa mkutano wa 30 wa IBF/USBA utakaofanyika katika jiji la Berlin, nchini Ujerumani Mai mwakani.
 Katika hatua nyingine:
 Bwama Michael Tetteh na bwana Henry Many-Spain wa GoldMike Promotions and Golden Concept za jiji la Accra, Ghana wameteuliwa kama promota wa mwaka 2012 wa mapambano ya IBF ya mabara. Bwana Tetteh amepromoti mapambano mengi ya IBF ya mabara (Continental Titles) kuliko promota mwingine yeyote katika bara la Afrika.
 Aidha, IBF imemteua bwana Branco Milenkovik wa kampuni ya Branco Sports Productions ya jiji la Johannesburg, nchini Afrika ya Kusini kama promota wake wa mwaka wa mapambano ya dunia mwaka 2012. Hii ni mara ya 3 mfululizo kwa Branco kuteuliwa kama promota wa mwaka kwa kuandaa mapambano mengi ya IBF ya ubingwa wa dunia.

No comments:

Post a Comment