CHEKA AWAAHIDI WATANZANIA USHINDI WA KISHINDO, MKANDA KUBAKI TANZANIA
Bondia wa kimataifa asiyepigika, Mtanzania
Francis mwana wa Cheka kutoka katika jiji lisilo na bahari la Morogoro
amewaahidi watanzania ushindi wa kishindo katika mpambano wake na bondia
kutoka Malawi Chimwemwe Chiotcha kesho tarehe 26 Desemba 2012 siku
ijulikanayo kama “Boxing Day”
Wababe hao walizuiwa na maofisa
wa ngumi wa TPBC na wale wa IBF kutozipiga kavukavu wakati walipokuwa
wanapima uzito kwenye hoteli ya nyota tane (5) ya Naura Springs ya
jijini Arusha leo tarehe 25 Desemba 2012.
Cheka amesema kuwa kazi yake ni
moja tu kumpiga Chiotcha kipigo kitakatifu ili akumbuke kuwa yeye ndiye
jogoo pekee la IBF katika bara la Afrika, Ghuba ya Uajemi na Mashariki
ya Kati.
Tayari Shirikisho la Ngumi la
Kimataifa (IBF) lenye makao yake makuu katika jiji la New Jersey kule
Marekani limeshatuma barua ya kuliruhusu pambano hilo kuwa la ubingwa wa
Afrika, Ghuba ya Uajemi na Mashariki ya Kati (IBF AMEGP).
Katika barua yake kwa promota wa
pambano hilo bwana Andrew George wa kampuni ya Green Hills (T) Limited,
Mwenyekiti wa Kamati ya Ubingwa wa IBF Lindsey Tucker alimtakia bwana
George mafaniko katika mpambano huo na kuwataja maaofisa wa ulingo
kutoka Tanzania kuwa wasimamizi wakiongozwa na Rais wa Shirikisho hilo
katika bara la Afrika, Ghuba ya Uajemi na Mashariki ya Kati, Mtanzania
Onesmo Ngowi.
Hii itakuwa mara ya tatu mwaka
huu wa 2012 kwa mkanda wa IBF kushindaniwa hapa Tanzania. Mara ya kwanza
ilikuwa mwezi wa Aprili mwaka huu wakati Francis Cheka alipopambana na
Mtanzania mwenzake Mada Maugo kugombea mkanda wa IBF katika bara la
Afrika uzito wa Super Middle.
Mwezi wa August 2012 Ramadhani
Shauri alikutana na Sunday Kizito kutoka nchini Uganda kugombea mkanda
wa IBF katika bara la Afrika uzito wa unyoya (Featherweight). Mapambano
hayo mawili yaliandaliwa na bwana Lucas Rutainurwa wa Kitwe General
Traders ya jijini Dar-Es-Salaam.
Mpambano wa mwezi huu wa Desemba
ni wa kufunga mwaka huu wa 2012 na utamkutanisha Francis Cheka na Luteni
usu wajeshi la Malawi Chimwemwe Chiotcha kugombea mkanda wa IBF katika
bara la Afrika, Ghuba ya Uajemi na Mashariki ya Kati uzito wa Super
Middleweight.
Mungu ambariki Francis mwana wa Cheka, Mungu aijalie Tanzania, Amina!
|
No comments:
Post a Comment