Utafiti uliofanywa hivi karibuni umeonyesha kuwa zaidi ya wajane 544
wametendewa vitendo vya kikatili, ikiwamo kubakwa na mashemeji zao
kuanzia Januari hadi Julai, mwaka huu.
Utafiti
huo unaonyesha kuwa kati ya hao, wajane 18 walirithiwa na kutakaswa
wakati nane walilazimishwa kuingiliwa kinyume cha maumbile kwa imani ya
kusafisha mikosi katika ukoo.
Taarifa
ya utafiti huo ilitolewa jana jijini Dar es Salaam na Mkurugenzi
Mtendaji wa Kituo cha Msaada wa Sheria kwa Wanawake na Watoto (WLAC),
Theodosi Muhulo. Alikuwa akitoa taarifa hiyo mbele ya waandishi wa
habari, iliyolenga kukemea vitendo vya kikatili na kibaguzi
vinavyoendelea dhidi ya wajane.
Muhulo
alisema utafiti uliofanywa na kituo umebaini kuwa baadhi ya wajane
wamekuwa wakiporwa ardhi na mali walizoachiwa na waume zao pindi
wanapofariki. Alisema utafiti huo ulifanywa kupitia kikosi kazi cha
kamati ya mkataba wa kimataifa wa kuondoa aina zote za ubaguzi dhidi ya
wanawake (CEDAW).
Alisema idadi hiyo ni kutoka katika vituo vya Dar es Salaam, Muleba, Karagwe, Kasulu Kigoma, Mara, Shinyanga na Songea.
“Takwimu
kutoka Mara zinaonyesha kuwa wajane 55 walinyang’anywa ardhi zao baada
ya waume zao kufariki, 23 walipewa mirathi kidogo, wajane 41 walifukuzwa
baada ya waume zao kufariki kwa maambukizi ya VVU. Takwimu hizi ambazo
ni za kuanzia Januari mpaka Julai 2012, pia zilijumuisha mashauri 174
kutoka Kitengo cha Wasaidizi wa Sheria, kilichopo Songea, yanayohusu
wajane kunyimwa haki zao,” alisema.
Kutokana
na hali hiyo, aliitaka Serikali kufanya marekebisho ya sheria za
mirathi kwa kuwa mfumo dume uliopo unabagua na kukandamiza wanawake na
kuchangia ukandamizaji wa kiuchumi.
“Vile
vile sheria hizi zinakinzana na sheria mama ambayo ipo katika Katiba ya
mwaka 1977 ibara ya 12, 13 na 24 pamoja na mikataba mbalimbali ya
Kimataifa, ambayo serikali yetu imeridhia. Mfumo huo wa mirathi unakiuka
haki ya msingi ya usawa, umiliki wa mali na kuwa na maisha bora,
familia na kutweza utu wa mwanamke, hususani wajane,” alisema.
Naye
Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Wanawake na Ustawi wa Mtoto (TWCWC),
Edda Mariki, alitoa wito kwa jamii kuondokana na mila potofu dhidi ya
wajane na kuwatendea haki badala ya kuwanyanyasa.
“Mashemeji
waache kubaka wajane kwa kutumia mfumo wa kurithi wajane, aidha jamii
iondokane na dhana ya kuona wajane ni wachawi na wengine kusababisha
kupigwa na kuuawa,” alisema.
Alizitaka
taasisi mbalimbali kuendelea kutoa elimu kwa Watanzania ili kuondokana
na mila potofu kwa ustawi wa jamii, kwani hicho ndiyo chanzo.