Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Nchi Kavu na Majini (Sumatra)
imetangaza kuhamisha kituo maarufu cha daladala cha Mwenge kwenda eneo
la Makumbusho.
Katika taarifa yake kwa vyombo vya habari jana, ofisa mfawidhi wa
Sumatra wa Kanda ya Mashariki, Conrad Shio alisema Kituo cha Mwenge
kitafungwa rasmi Jumapili na eneo hilo litabaki wazi kupisha upanuzi wa
Barabara ya Ali Hassan Mwinyi. Shio alieleza sababu ya kuhamisha kituo
hicho kuwa ni ufinyu wa eneo lenyewe jambo linalosababisha magari
kushindwa kuingia kituoni hapo kwa wakati, hasa nyakati za asubuhi na
jioni. Hali hiyo husababisha foleni kubwa isiyo ya lazima.
Alisisitiza madereva wote kutii agizo hilo kuanzia Jumatatu na kwamba
atakayekiuka agizo hilo atachukuliwa hatua kali za kisheria. Pia,
aliwataka abiria kutolazimisha kushushwa katika eneo hilo wakati hakuna
kituo. Shio aliongeza kuwa barabara za kuingia na kutoka Kituo cha
Makumbusho bado zinakarabatiwa na Manispaa ya Kinondoni ili kurahisisha
uingiaji na utokaji wa magari katika kituo hicho.
Hivi karibuni, madereva wa daladala zinazofanya safari kati ya Mwenge,
Tegeta na Ubungo waligoma kutoa huduma kushinikiza Serikali kueleza
kituo mbadala baada ya kufungwa kwa kituo cha Ubungo kutokana na ujenzi
unaoendelea wa barabara.
No comments:
Post a Comment