DAKTARI NGULI WA KUTOA MIMBA ANASWA DAR...!SOMA ZAIDI HAPA...
MWAKA
umeanza, mambo mapya pia yapo! Oparesheni Fichua Maovu ‘OFM’ ya Global
Publishers imeingia kazini kwa kasi zaidi. Safari hii imemnasa daktari
anayejulikana kwa jina moja la Mambo maarufu sana kwa jina la Dokta
Mambo katika jaribio linalodaiwa kuwa ni la utoaji mimba.
Tukio hilo lilitokea katika zahanati yake (jina lipo) iliyopo Kawe
jijini Dar es Salaam ambapo daktari huyo anayejulikana sana na wateja
wake, hasa akina mama alipoingiliwa na OFM wakishirikiana na polisi
baada ya kumuwekea mtego wa mbinu za kishushushu.
MALALAMIKO YA AWALI
Mwishoni mwa Desemba, mwaka
jana, mtu mmoja (jina lipo) alituma ujumbe mfupi wa maneno (SMS) kwenda
OFM akimlalamikia dokta huyo kwamba amekuwa na mchezo wa kutoa mimba
wanawake wakiwemo mabinti wa shule, kitendo alichodai haoni kama ni
sawa.
“Naitwa….(jina lipo), nilikuwa naishi Kawe lakini kwa sasa nimehamia
Mbezi (hakusema Mbezi gani). Kama hapo ni OFM (Oparesheni Fichua Maovu)
naomba mumshughulikie daktari mmoja anaitwa Dokta Mambo wa Kawe. Huyu
daktari jamani amekuwa na tabia ya kutoa mimba wanawake hata wasio na
matatizo.
“Ninavyojua mimi hakuna hospitali inayoruhusiwa kutoa mimba Tanzania,
labda pale ambapo itathibitika kwamba mjamzito ana kifafa, kwa hiyo
hatari inakuwepo ya kumpoteza mama au mtoto tumboni ndiyo mimba
hutolewa. Wananchi wa Kawe wamekilalamikia kitendo hicho hadi wamechoka.
Polisi Kawe wamemshindwa,” alisema raia mwema huyo.
OFM YAANZA KAZI
Baada ya kupokea tuhuma hizo, OFM
ilijipanga na kuingia kazini. Ilimwandaa paparazi wa kike na
kumtengenezea ujauzito wa bandia na paparazi wa kiume ambaye ni mchumba
wake (wa bandia) ili kwenda naye kwa Dokta Mambo kuona kama kweli
anajihusisha na kazi hiyo au la!
JUMANNE, DESEMBA 31, 2013
Ilikuwa Jumanne ya
Desemba 31, 2013, OFM na paparazi huyo walitia timu kwenye zahanati hiyo
na kukutana na dokta huyo ambaye alikubali kumtoa ujauzito paparazi
huyo.
‘Mchumba’ wa paparazi huyo alimwambia dokta kwamba
wamekubaliana kuitoa mimba hiyo kwa sababu ya hali ya uchumba, daktari
akasema haina shida.
AWEKA MASHARTI MAGUMU
Katika hali ambayo OFM
hawakuitarajia, daktari huyo alisema kwa kawaida kabla hajamchoropoa
mimba mteja wake lazima aipime kwanza ili kujua ina muda gani.
Zoezi
hilo lilikuwa gumu kwa OFM kwa sababu paparazi huyo hakuwa na ujauzito.
Ilibidi ‘wateja’ hao waondoke kwa kisingizio kwamba wanakwenda kujipanga
kwa fedha aliyoitaka ambayo ni shilingi laki moja na kwamba wangerudi
siku iliyofuata (Jumatano).
OFM WAJIPANGA UPYA
‘Wachumba’ hao waliondoka na
kuungana na Timu ya OFM ambayo ilikuwa mahali imekaa mkao wa mtego.
Baada ya kupata simulizi za ndani ya zahanati hiyo, OFM ilirejea ofisini
na kumweleza kamanda mkuu wake ambaye alikaa na timu hiyo na kupanga
mpango mpya.
“Bosi, Dokta Mambo ameshakubali, lakini sera zake ni kwamba hawezi
kumtoa mimba mjamzito hadi ampime kwanza na kujua ina miezi mingapi.
Sasa huyu (paparazi) hana ujauzito, tungekubali ampime tungeumbuka,
tukamwambia tunakwenda kusaka fedha kwanza,” OFM mmoja alimwambia
kamanda mkuu.
OFM YATUMWA MTAANI KUSAKA MWENYE MIMBA YA UKWELI
Kamanda
Mkuu wa OFM (jina lipo) aliagiza timu yake kuingia mtaani ili kumsaka
mwanamke mwenye mimba ya ukweli ambaye ndiye angekuwa na sifa za
kutolewa ujauzito na daktari huyo.
Hayo yote yalifanyika baada ya pia
uchunguzi wa kina kufanyika maeneo ya Kawe kuhusu tabia ya daktari huyo
na kudaiwa kuwa, hawezi kuacha ‘kamchezo hako ka siku nyingi’.
Mjamzito wa kweli alipatikana (jina lipo), akiwa na mimba ya miezi
mitatu. Akashirikishwa katika zoezi hilo ambapo hata yeye aliumia
kusikia kwamba kuna daktari anayetoa mimba wanawake hata wale ambao
hawana sababu za kufanya hivyo kama sheria za utabibu zinavyotaka.
WATINGA POLISI KAWE
Baada ya kupatikana kwa
mjamzito huyo, OFM ilimchukua hadi Kituo cha Polisi Kawe, Dar es Salaam
na kuwaambia wahusika kuhusu tabia ya daktari huyo inayolalamikiwa na
watu ili ikibidi watoe askari kwa kuungana na OFM kwenda kumtia nguvuni.
POLISI KAWE WAONESHA ‘MAAJABU’
Katika hali ya
kushangaza, polisi wa kituo hicho, awali waliwataka OFM watoke nje ili
wajadili wao. Baadaye waliwaita na kusema kwamba hawawezi kutoa polisi,
kama ishu ni daktari huyo kulalamikiwa na watu, watamwita na kumkanya
aache mchezo huo!
“Hatuwezi kushirikiana nanyi katika hilo zoezi, kama ni kweli kuna
hayo maneno ya watu, sisi tutamwita tumuonye aache mara moja,” alisema
mmoja wa askari wa Kituo cha Kawe.
Katika hali iliyoshangaza zaidi, polisi hao waliwataka waandishi wote
walio kwenye msafara kuandika maelezo ya malalamiko kuhusu daktari huyo
kwenye kitabu cha ripoti kituoni hapo (Report Book ‘RB’).
Maelezo yaliandikwa. Jina……, umri…., makazi…., kazi…., dini….. na aina ya malalamiko. Baada ya hapo wakatakiwa kuondoka zao.
OFM WARUDI KWA DOKTA MAMBO
Januari 3, 2014, OFM
wakiwa na mjamzito wa kweli walikwenda kwa dokta huyo ambapo kama
ilivyo utaratibu wake, alimpima kwanza na kutoa majibu kwamba ana mimba
ya miezi 3 na wiki mbili, akasema ni kubwa sana, hivyo zinatakiwa
shilingi 160,000.
Hata hivyo, mchumba mtu alisema hana kiasi hicho cha pesa. Ikatokea
vuta nikuvute hadi kufikia shilingi 100,000. Ikumbukwe kwamba, mpaka
hapo Dokta Mambo hakuwa anajua kwamba mchezo wa pili ni uleule wa
kwanza.
“Basi dokta tunaomba tuje kesho na hiyo laki moja,” mchumba mtu
alimwambia daktari huyo ambaye alikubali huku na yeye akiomba kuwa, hiyo
kesho iwe saa kumi na moja jioni.
OFM, POLISI, MJAMZITO NA MCHUMBA’KE
Kesho yake
ilifika, OFM ikiwa na mjamzito huyo akiwa na mchumba’ake walikwenda
maeneo ya Kawe jirani na zahanati ya Dokta Mambo kujaribu kupanga namna
ya kufanikisha oparesheni hiyo.
Bado tatizo lilikuwa uwepo wa polisi baada ya kubaniwa na wale wa
Kawe. Mungu si Athumani, wakiwa wanashangaashangaa eneo, ilipita
pikipiki ya askari wa doria ‘Tigo’ na mara moja OFM ikawasimamisha.
Bila kupoteza muda, OFM waliwaeleza polisi wale mchezo mzima
ulivyokuwa na kwamba walihitaji msaada wao ili kufanikisha zoezi hilo,
walikubali bila kinyongo na mara moja wakaongozana hadi eneo la tukio.
OFM mmoja kati yao aliingia ndani ya zahanati hiyo akijifanya
amekwenda kupima malaria, wale polisi wawili na OFM wengine walikaa
mafichoni kutega mingo, wachumba nao waliingia mpaka kwa dokta wakiwa na
kitita cha shilingi laki moja mkononi.
MJAMZITO APELEKWA CHUMBA CHA KAZI
Baada ya
kuwapokea na kutoa kiasi hicho cha pesa, mjamzito huyo alipelekwa chumba
kinachodaiwa ni cha kutolea mimba huku mchumba mtu akikaa kwenye fomu
kusubiri matokeo.
UTAALAM WA OFM
Kilikuwa kipindi kinachotaka
mawasiliano ya hali ya juu, OFM ikitambua kuwa kosa moja goli moja,
walikuwa makini kwa mawasiliano. Mjamzito chumbani kumwambia mchumba
wake kwenye fomu, naye kuwaambia OFM wa nje hatua kwa hatua.
Katika mazingira hayo, hakuna OFM aliyetakiwa kupokea simu wala kutuma meseji kwa mtu asiyehusiana na kazi hiyo.
TUKIO LANASWA
Ilikuwa wakati daktari huyo akiwa
na glovsi mikononi, mjamzito wa kweli akiwa kitandani na nesi mmoja wa
kumsaidia daktari wakiwa ndani ya chumba, ndipo OFM na polisi
walipovamia na kunasa tukio ambalo lilionekana dhahiri kwamba lilikuwa
jaribio la kutoa mimba.
Hapo ndipo Dokta Mambo alipogundua kuwa kumbe ‘kazi’ aliyopewa
ilikuwa feki na wale walikuwa makamanda wa OFM wakishirikiana na polisi
waaminifu, wazalendo na wanaopenda kazi yao sawasawa.
KWA NINI?
Lilikuwa jaribio la kutoa mimba kwa
sababu, ndani ya chumba zilikutwa zana za shughuli hiyo huku mjamzito
akiwa kitandani tayari kwa kufanyiwa mchakato.
Huku OFM wakimpiga picha (zipo za kumwaga kwenye maktaba yetu –
ukitaka kuziona njoo Bamaga), askari nao wakichunguza mazingira zaidi na
kukamata vifaa, daktari huyo alinywea huku msaidizi wake akitokwa
machozi.
POLISI WAMWINGIZA NDANI YA GARI
Zoezi hilo
lilikamilika kwa daktari huyo kuchukuliwa na askari hao ambao walikodi
gari, mmoja akawa na dokta garini akiwa na vifaa vyake chini ya ulinzi,
mwingine akiwafuata kwa nyuma na pikipiki.
Askari hao, waliwaeleza OFM kuwa wataitwa Kituo cha Polisi Oysterbay kwa ajili ya kuandika maelezo.
Risasi
Mchanganyiko lilimtafuta kwa njia ya simu Kamanda wa Mkoa wa Kipolisi
Kinondoni, ACP Camillius Wambura ili kujua kama suala hilo limefika
mezani kwake, lakini simu yake haikupatikana muda wote ilipopigwa.
Hata lilipomtafuta Kamanda wa Polisi wa Kanda Maalum ya Dar es
Salaam, CP Suleiman Kova ili limsimulie mchezo mzima ulivyokuwa, naye
hakupatikana hadi tulipokwenda mitamboni.
Bado tunaendelea kuwatafuta viongozi wa polisi na ukweli wa kina
kuhusu namna ishu hiyo inavyoendelea, tunawajulisha katika matoleo yetu
yanayofuata
No comments:
Post a Comment