ZITTO AJIBU TUHUMA ZA YEYE KUPOKEA MABILIONI KUTOKA CCM
TAMKO rasmi la Ndugu Zitto Z. KABWE (MB) kuhusiana na kinachoitwa "Taarifa ya Siri ya Chadema"
Ndugu Wanahabari,
NILIPOKUWA
katika ziara ya bara la Ulaya kati ya Oktoba 21 mpaka Novemba 2 mwaka
huu (2013), nilipokea kwa njia ya barua pepe ripoti inayoitwa "Taarifa
ya Siri ya Chadema" ambayo pia ilikuwa imesambazwa katika mitandao
mbalimbali ya kijamii.
“Taarifa
ya Chadema inasema kwamba chama hicho (chama changu) kilikuwa
kimechunguza mwenendo wangu tangu mwaka 2008 hadi 2010 na kubaini kuwa
mimi napokea fedha kutoka Chama Cha Mapinduzi (CCM) ili kuivuruga
Chadema.
Ripoti
hiyo ilinihusisha pia na mwananchi raia wa Ujerumani, Andrea Cordes
ambaye, kwa mujibu wa ripoti hiyo, alinisaidia kupokea na kuhifadhi
kiasi cha dola 250,000 za Marekani kupitia kwenye akaunti yake binafsi.
Taarifa hii ya kutunga na iliyojaa uongo wa kiwango cha kutisha, imenifadhaisha, kunisikitisha na kunikasirisha.
Taarifa
hii iliibuliwa katika kipindi ambacho nilikuwa safarini kutetea haki za
Watanzania na Waafrika ambao utajiri wao wa rasilimali unafaidiwa na
watu wachache waliohifadhi mali katika nje za nje na pia kupigania
makampuni ya mataifa tajiri yalipe kodi stahiki katika nchi zetu.
Pengine
lengo la ripoti hiyo lilikuwa ni kutaka kunipoteza kutoka katika nia na
dhamira yangu ya dhati ya kutaka Watanzania wafaidike na utajiri wao.
Muda ambao watunzi wa ripoti hiyo waliamua kutoa taarifa yao unazua
maswali mengi kuliko majibu.
Nafahamu
kwamba mimi ni mwanasiasa ambaye nimekuwa mlengwa (target) wa
mashambulizi kutoka kwa makundi mbalimbali ya wanasiasa na vikundi vyao.
Kama mwanasiasa, niko tayari kupokea changamoto zozote zinazokuja na
uanasiasa wangu.
Hata
hivyo, ambacho sitakubali ni kwa watu kutumia jina langu na uanasiasa
wangu kunichafua mimi binafsi na watu wengine wasiohusika kwa sababu ya
kutaka kutimiza malengo yao ya kidhalimu.
Raia huyo
wa Kijerumani tayari amekana kuhifadhi fedha zangu. Kwa maelezo yake
kwa baadhi ya viongozi wa Chadema amekana kuwa na akaunti inayotajwa na
amekana pia kuwepo nchini Ujerumani katika siku na wakati uliotajwa
kwenye ripoti hiyo.
Ripoti
hiyo imemtaja pia mtu kama Dk. Charles Kimei, Mkurugenzi Mtendaji wa
Benki ya CRDB ikidai kwamba nilikutana naye na alishiriki kwenye igizo
hilo la kunipa fedha.
Niseme
mapema kwamba tangu kuzaliwa kwangu sijawahi hata mara moja kukutana na
Dk. Kimei popote pale ndani au nje ya nchi. Kumuingiza mtu ambaye
amejenga jina lake kwenye taaluma ya kibenki kwa sababu tu ya lengo ovu
la kumchafua Zitto Zuberi Kabwe si uungwana bali ni unyama.
Kutokana
na uchafuzi huu wa wazi dhidi ya taswira yangu binafsi na watu wengine
walioingizwa kwenye mkumbo huu, nimeandika rasmi kwa Katibu Mkuu wa
Chadema, Dk.Wilbrod Slaa kumwomba athibitishe kwamba kinachoitwa Taarifa
ya Siri ya Chadema ni kweli ni taarifa ya chama au kiikanushe ili
niweze kuchukua hatua za kisheria dhidi ya waandishi wa hekaya hiyo.
Cha
ajabu, nimepokea ujumbe wa kutishiwa maisha kutoka kwa mtu anayejiita
Theo Mutahaba na kuahidiwa KUPOTEZWA endapo nitaendelea na jitihada
zangu za kupambana na ufisadi na kutafuta haki kwa Watanzania wote
pasipo kujali tofauti zao za kiitikadi, kikanda, kikabila na kidini.
Natarajia
kuchukua hatua kali za kisheria dhidi ya wote ambao wamehusika na
utungaji na uenezi wa taarifa hii. Nitahakikisha kwamba wahusika
wanatafutwa na kufunguliwa mashitaka stahiki ya upotoshaji na
kuchafuana.
Ni
matarajio yangu kwamba wale wenye mapenzi mema na Tanzania, mimi binafsi
na utawala wa sheria, wataelewa nia yangu ya kutafuta haki katika suala
hili.
Nimeamua
kujitolea maisha yangu kwa ajili ya Watanzania na kama alivyopata kusema
Rais Mstaafu wa Afrika Kusini, Nelson Mandela; “Struggle Is My Life.”
Forward Ever, Backward Never- Kwame Nkrumah
Zitto Kabwe (Mb)
10/11/2013
No comments:
Post a Comment