MMOJA
wa mawaziri wa Serikali ya Awamu ya Tatu na mbunge anayetoka Mkoa wa
Tabora, anatuhumiwa kumbaka na kisha kutishia kumuua msichana yatima
mwenye umri wa miaka 16 anayesoma Shule ya Sekondari Turiani iliyoko
Magomeni jijini Dar es Salaam.
Waziri huyo (jina lake
linahifadhiwa kwa sasa), ametoa tishio hilo la mauaji kwa njia ya ujumbe
mfupi kupitia namba iliyosajiliwa kwa jina lake kwa kile alichodai
kukaidi amri ya kutaka wasifichue uchafu wake kwa waandishi wa habari.
Akizungumza
kwa uchungu na gazeti la Tanzania Daima, mwanafunzi huyo alisema kuwa
waziri huyo alimbaka kwenye hoteli moja ya kitalii iliyoko jijini Dar
es Salaam mwaka 2011, na kurudia tena kitendo hicho katika Jengo la
Biashara Complex lililoko Mwananyamala Juni 3, 2012.
Mwanafunzi
huyo alisema alifikwa na ukatili huo alipoitwa na kiongozi huyo kwenda
kuchukua fedha za ada na matumizi mengine, ambapo mara ya kwanza alimpa
sh 700,000 na mara ya pili sh 350,000.
Yatima huyo anayeishi na
dada yake, alikutanishwa na waziri huyo wa zamani na baba wa mwanafunzi
mwenzake, kutokana na msaada mkubwa aliompa akiwa mgonjwa, ili aweze
kumsaidia fedha za ada kama ishara ya shukurani.
Mwanafunzi huyo
alisema baada ya kutambulishwa, aliitwa katika hoteli hiyo ambako baada
ya kufika mapokezi wafanyakazi walimkataza kuingia chumbani kutokana na
umri wake kuwa mdogo (mwaka 2011 alikuwa na miaka 14), lakini waziri
huyo wa zamani aliamrisha aruhusiwe.
Akiwa chumbani, mwanafunzi
huyo alilazimishwa kulala naye kisha kumpa sh 700,000, badala ya
shilingi 67,000 alizohitaji kwa ajili ya ada.
Mwanafunzi huyo
alisema baada ya muhula mmoja aliitwa tena na kiongozi huyo katika Jengo
la Biashara Complex lililoko Mwananyamala Juni 3, 2012, ambapo pia
alimlazimisha kulala naye kwenye zulia la ofisi yake, kisha kumpa sh
350,000.
Mwanafunzi huyo alisimulia kwamba wakati anatoka kwa
huzuni ofisini kwa mbunge huyo, mmoja wa wahudumu alimuuliza sababu ya
huzuni yake na akalazimika kumweleza kisa hicho, ndipo mhudumu alitokwa
machozi huku akimwambia kwamba, atakufa kwa sababu “baba huyo ni muathirika wa ukimwi”.
Aliongeza
kuwa baada ya kuambiwa vile alilia na kufanya fujo hapo mapokezi, hadi
alipokamatwa na walinzi, kisha kupelekwa kituo cha polisi kufunguliwa
mashitaka.
Hata hivyo, alisema polisi waliposimuliwa kisa chote,
walilazimika kumwita waziri huyo wa zamani na alipofika alikiri na
kuomba mambo yaishie hapo.
“Alikubali na akaahidi kunilipia ada
na pesa za matumizi kiasi cha sh 300,000 kila mwezi, jambo ambalo
amekuwa akilitekeleza kupitia simu yake ya mkononi (namba za simu
tunazo),” alisema.
Kwa mujibu wa mwanafunzi huyo, Januari 24,
mwaka huu walitishiwa maisha na kiongozi huyo, lakini mwezi uliofuata,
mtu asiyefahamika alienda nyumbani kwao na kuacha gari (namba tunazo)
aina ya Mercedes Benz yenye rangi ya bluu wakati akiwa shuleni, kisha
kuacha ufunguo kwa jirani yao kwa maelekezo kuwa akifika apewe.
Wamesema
baadaye kiongozi huyo aliwapigia simu kuwaarifu kuwa amempa zawadi ya
gari kwa ajili ya matumizi, na wanaruhusiwa kuliuza ili wapate pesa za
mahitaji yake siku zilizosalia, kwani baada ya uchaguzi mkuu 2015,
atakuwa Waziri Mkuu, hivyo itakuwa ngumu yeye kumtumia huyo binti pesa
kama alivyoelekezwa na Jeshi la Polisi kituo cha Oysterbay.
Hata hivyo, wasichana hao walishindwa kulitumia gari hilo hivyo kutoa taarifa polisi ili kesi ipelekwe mahakamani.
Wamedai
kuwa polisi walikubali kulipeleka tatizo hilo kwa katibu wa Bunge,
ambaye alimwita mwanafunzi huyo na nduguye Dodoma kukutana na Kamati ya
Haki na Maadili ya Bunge.
Hata hivyo, walipofika Dodoma
hawakuweza kupata ufumbuzi kwa maelezo kuwa waziri huyo wa zamani
hakuwepo hadi Bunge lilipoisha. Kwa muda wote, wasichana hao walisema
waligharimiwa kila kitu na Ofisi ya Bunge.
Kabla ya kurudi Dar es
Salaam, mabinti hao walisema waliitwa na kiongozi mmoja wa juu wa CCM
aliyewalekeza kwenda kumwona Makamu Mwenyekiti wa chama hicho, Philip
Mangula.
Kwa mujibu wa mawasiliano, kiongozi mwingine (jina
tunalo) alimpigia binti huyo simu majira ya asubuhi, akimtaka aende
ofisi za CCM, lakini hakupata msaada wowote zaidi ya kuombwa asubiri
hadi wakati wa kipindi cha Bunge ili apate msaada kwa kuwa ni suala
binafsi.
Hata hivyo, wakati akiwa njiani kuelekea katika kituo
kimoja cha runinga kwa ajili ya kutoa kilio chake, mwanafunzi huyo na
dada yake walifuatiliwa na watu wasiowajua, jambo lililowalazimisha
kuomba msaada wa wapita njia.
Hata alipofika katika ofisi za
kituo hicho cha runinga, watu watatu akiwemo mwanamke mmoja walifika
wakidai kuwa ndugu wa wasichana hao na kuwakataza waandishi wasikubali
kusikiliza neno lolote, wakati sio kweli.
Aidha, walitumiwa
ujumbe kutoka katika namba ya mmoja wa wafanyakazi wa makao makuu ya
CCM, akiwasihi kufumba mdomo kwa kuwa anawapenda na hataki wadhurike.
Baada
ya jitihada za kuwanyamazisha wasichana hao kushindikana, ndipo
mwathirika alipoanza kupokea ujumbe wa kutishia maisha kupitia katika
namba ya simu ya 078499…. Ikisema: “Waandishi hawatakusaidia kamwe,
Bunge la Katiba likianza watu watakusahau kama uliuawa.
Mtasahaulika
kabisa, subirini mje mzikwe leo usiku kwenu, sitanii, hakuna wa
kunifanya lolote, serikali ndio sisi, salini kabisa.”
Jitihada za
kumpata waziri huyo wa zamani na mbunge wa CCM, ziligonga mwamba. Mara
ya kwanza simu yake moja ilipokelewa na mtu aliyejitambulisha kama
dereva wake, na akataka aambiwe sababu za kumuhitaji kiongozi huyo.
Hata
aliposisitizwa kuwa anayehitajika ni mkubwa wake, alitoa namba nyingine
ya kumpata, lakini ilikuwa ikikatwa mara zote ilipokuwa ikiita.
Mbali
ya ujumbe huo wa vitisho, binti huyo alikuwa akitumiwa ujumbe
mbalimbali na watu asiowafahamu, na wengine kumpigia simu wakimwambia
wanajua amejificha wapi na kwamba hawezi kutoka.
Naibu Spika wa
Bunge, Job Ndugai, alipoulizwa kuhusiana na tuhuma hizi nzito,
alionyesha kushangaa na kuhoji; “na wewe umeanza kuandika mambo kama
haya?”
“Hilo ni jimbo binafsi zaidi na mimi siwezi kuongea lolote,” alisema na akakata simu.
Tanzania Daima Jumatano, liliwasiliana na Mbunge wa Kilindi, Beatrice Shelukindo, ambaye anadaiwa kulielewa vema suala hilo.
Shelukindo,
hata hivyo, licha ya kukubali kuwa alikuwa anajua tatizo hilo, aliomba
asiongee kwa kirefu kwa madai kuwa alikuwa kwenye kikao.
Kamanda
wa zamani wa polisi Mkoa wa kipolisi wa Kinondoni, Charles Kenyela
alipulizwa namna alivyoshughulikia jambo hilo, alikana kujua chochote
kwa madai kwamba, mambo kama hayo yanashughulikiwa na dawati maalumu.
Credit: Tanzania Daima
No comments:
Post a Comment