HATIMA ya Mbunge wa Urambo Magharibi Juma Kapuya (CCM), anayetuhumiwa
kutishia kumuua binti anayedaiwa kumbaka, amerejea nchini jana akitokea
nchini Sweden, huku Jeshi la Polisi likikwama kumtia mbaroni kama
lilivyokuwa likitamba.
Wakati mbunge huyo akiwasili nchini na kupokewa na kusindikizwa na
wapambe wake, Bunge limeridhia kukamatwa kwake kwani tuhuma
zinazomkabili ni za jinai na zinamhusu yeye binafsi.
Mbunge huyo ambaye amepata kuwa waziri, amerejea nchini jana majira
ya saa tano asubuhi kwa ndege ya Shirika la Qatar na kutua katika uwanja
huo wa ndege na kuondoka kupitia mlango wa watu maarufu (VIP).
Habari zinasema mbunge huyo alipoondoka katika Uwanja wa Ndege wa
Mwalimu Julius Nyerere alikwenda moja kwa moja kwenye moja ya hoteli za
jijini Dar es Salaam na kuacha mizigo yake, kisha kuondoka na gari namba
T 104 AEZ Toyota, huku wapambe wake wakiwa katika gari namba T 170 BGY
aina ya Benz.
Wakati Kapuya akitua katika uwanja huo wa ndege, polisi ambao kwa
takriban wiki moja sasa wamekuwa wakitamba kutaka kumtia mbaroni mara
baada ya kutua, baadhi yao walionekana wakisalimiana naye kama vile
hawakuwa wanamuwinda.
Tangu Profesa Kapuya alipoondoka nchini huku akizongwa na kashfa ya
kutishia kumuua binti anayedaiwa kumbaka, polisi wamekuwa wakitamba
kutaka kumtia mbaroni na kuahidi kuwa mara baada ya kurejea nchini
mbunge huyo angekuwa chini ya ulinzi.
Tanzania Daima juzi liliripoti mkakati wa polisi kutaka kumtia mbaroni
mbunge huyo mara atakapotua kwenye Uwanja wa Ndege wa Mwalimu Julius
Nyerere jijini Dar es Salaam.
Habari kutoka ndani ya Jeshi la Polisi zilisema kuwa kumekuwa na
shinikizo kutoka ndani na nje ya jeshi hilo kutaka waziri huyo wa zamani
ahojiwe kuhusiana na tuhuma zinazomkabili za kutishia kumuua binti
anayedaiwa kumbaka.
Hatua ya polisi kutaka kumnasa Kapuya akiwa uwanja wa ndege inadaiwa
kuchangiwa na taarifa ya wiki iliyopita kwamba baadhi ya
vigogo wa jeshi hilo walishiriki kufanikisha safari ya mbunge huyo nje
ya nchi huku wakijua fika anatakiwa na polisi.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, Camilius Wambura, alipoulizwa
kuhusu ujio wa Kapuya na kisha kuendelea kuachiwa huru, alisema yuko nje
ya Jiji la Dar es Salaam na hakuwa na taarifa za kurejea kwake.
Hata hivyo Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, Yusuph Mrefu,
alipoulizwa kuhusu sakata la Kapuya, alisema hakuwa na taarifa ya kile
kinachoendelea, kwa kuwa ndiyo kwanza amekabidhiwa ofisi.
“Mimi niambie jambo jipya, hapa ofisini ndiyo leo nimeingia kukaimu,
sasa hayo mambo nitayajulia wapi, ni vema ungeniambia jambo jipya tuweze
kutatua,” alisema Mrefu.
Kwa upande wake, Bunge limesema kuwa sakata la Profesa Kapuya
lilifikishwa bungeni na kubaini kuwa ni la jinai, hivyo linapaswa kwenda
kwenye mkondo wa kisheria.
Akizungumza na Tanzania Daima jana, Katibu wa Bunge, Thomas Kashilila,
alithibitisha kulifahamu suala hili, kwani binti aliyedai kubakwa na
kutishiwa kuuawa na mbunge huyo alikwenda bungeni wakati Bunge la 13
lilipokuwa likiendelea mjini Dodoma.
“Suala la binti huyo lilifikishwa ofisini kwangu kupitia kwa msaidizi
wangu ambaye alisikiliza hoja na rai yake na kushauriwa kuwa hilo ni
suala la jinai na linapaswa liende katika mkondo wa kisheria, hata hivyo
binti huyo alitambulishwa kwa Spika kama kiongozi wa wabunge na
kuelekeza kuwa tumshauri alifikishe katika mamlaka husika,” alisema
Kashilila.
Tayari binti anayedaiwa kubakwa na kutishiwa kuuawa ameshafungua
jalada namba OB/RB/21124/13 katika Kituo cha Polisi Oysterbay, jijini
Dar es Salaam na Jeshi la Polisi likaahidi kumkamata Kapuya popote alipo
ili kujibu tuhuma hizo zinazomkabili.
Tayari makachero wa polisi wameanza kufuatilia namba ya simu
inayodaiwa kutumika kumtisha binti huyo na wakati mwingine kutumika
kurusha pesa kwa njia ya mtandao, zinazodaiwa kutoka kwa Profesa Kapuya
kwenda kwa binti huyo.
No comments:
Post a Comment