Aliyekuwa Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chama cha demokrasia na Maendeleo (Chadema), Dk. Kitila Mkumbo, amemshambulia kwa maneno na kumrushia vijembe Mbunge wa Iramba Magharibi (CCM), Mwigulu Nchemba, kuwa kauli ya kumpa pole baada ya kusikia amevuliwa uongozi ni kiherehere.
Dk. Kitila alitoa kauli hiyo juzi mbele ya waandishi wa habari jijini Dar es Saalam, baada ya kutoa tamko lake kufuatia hatua ya chama chake ya kumvua nafasi za mamlaka ndani ya Chadema.
“Nimeshangaa kusikia Nchemba ananipa pole ilihali hakuna siku aliyowahi kunipongeza, mara zote amekuwa akisema usomi wangu ni wa ovyo… hiki kuherehere cha kunipa pole kimetoka wapi?” alihoji Dk. Mkumbo.
Alisema pamoja na kiherehere hicho cha Nchemba, bado msimamo wake ni dhahiri kwani mwaka 2015 ukifika atapambana naye iwe akiwa mwanachama wa Chadema au vinginevyo.
“Napenda kumtumia salama kuwa niwe mwanachama nisiwe, niwe Chadema au nje ya Chadema, ajue lazima nimng’oe kwenye uchaguzi mkuu ujao hakuna mchezo kwenye hilo, nimedhamiria
Nchemba amekuwa akituhumiwa na Chadema kwa kuwatunia wanachama kadhaa ambao wamekuwa wakifanya vitendo vya kukisaliti chama pamoja na waliofukuzwa kutokana na tuhuma kadhaa.
CHADEMA KUFAFANUA LEO
Wakati huo huo, Chadema kimesema kitatoa ufafanuzi wa kauli walizoziita za uzushi na upotoshaji mkubwa uliofanywa na waliovuliwa uongozi ndani ya chama hicho.
Waliovuliwa uongozi ni aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu, Zitto Kabwe, Dk. Kitila Mkumbo na aliyekuwa Mwenyekiti wa Mkoa wa Arusha, Samson Mwigamba.
Zitto na Dk. Mkumbo juzi walizungumza na waandishi wa habari kujibu tuhuma zilizoelekezwa kwao na kusababisha kuvuliwa uongozi na kupewa siku 14 wawe wamejieleza kwa chama.
Ofisa Habari wa Chadema, Prosper Makene, alisema jana kuwa mkutano baina ya viongozi wa chama hicho na waandishi wa habari utafanyika leo kwenye ofisi za chama hicho.
Alisema lengo la mkutano huo ni kueleza maamuzi mbalimbali yaliyofanywa na CC ikiwa ni pamoja na kueleza hali ya siasa ndani na mahusiano ya kimataifa ambayo ilikuwa moja ya ajenda kwenye kikao.
“Tutatumia fursa hiyo kutoa ufafanuzi dhidi ya kauli za uongo na upotoshaji zilizotolewa kwa vyombo vya habari na Zitto na Dk. Mkumbo,” alifafanua Makene.
Alisema mambo yaliyojadiliwa na kufanyiwa maamuzi ya CC ni ya msingi hivyo Watanzania wanapaswa kujulishwa na uongozi wa chama hicho utafanya hivyo.
Juzi Zitto na Kitila wakiwa wameafuatana na wapambe wao na ndugu, na mwanasheria wa chama na diwani wa kata ya Mabogini wilayani Moshi Vijijini, Albert Msando, walitoa ufafanuzi na msimamo wao dhidi ya maamuzi ya CC.
Dk. Mkumbo, alikiri kushirikiana na Mwigamba, kuandaa waraka uliokuwa na mkakati wa kupata Mwenyekiti wa taifa wanayemtaka.
Alitoboa siri hiyo na kusema mtu ambaye kwenye waraka walimtambulisha kama MM kuwa ni Zitto Kabwe na ndiye waliyekuwa wanamuandaa kuwania nafasi ya Mwenyekiti wa taifa, M1 ni Mwigamba na M2 ni yeye. (Soma waraka huo ukurasa wa 9).
Dk. Mkumbo alitetea waraka wao kuwa umefanya tathmini ya kisayansi (SWOT analysis) kwa maana ya kujua uimara, udhaifu, nafasi au fursa na hatari ya mgombea wanayemuandaa dhidi ya anayepambana naye ili kujipanga.
“Kwenye waraka wetu ambao Zitto hakuufahamu, tumeeleza madhaifu saba ya tunayeona anafaa kuwa Mwenyekiti, mfano tumeeleza MM maneno yake mara nyingi hayazingatii anazungumza katika mazingira gani na hivyo kuwasha masikio ya wanataasisi na kumfanya asikubalike…huu ni udhaifu, tumeainisha udhaifu takribani saba ili kuyashughulikia ukishajua, unajua unatumia njia gani kufunika,” alibainisha.
Kwa upande wake Zitto, alisema hana mpango wa kukihama chama na atakuwa wa mwisho kufanya hivyo kwa hiari yake.
Alisema kinachoendelea ndani ya chama hicho ni mapambano ya kukuza demokrasia, mapambano baina ya wapenda demokrasia dhidi ya waafidhina, waumini wa uwajibikaji dhidi ya wabadhirifu na wapenda siasa safi dhidi ya watukuzao siasa majitaka.
Baadhi ya tuhuma alizofafanua ni kuwa amekidhalilisha chama kwa tamko la Kamati ya kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) kwamba hesabu za vyama hazijakaguliwa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) na kwamba alipaswa kuwasiliana kwanza na uongozi wa chama ‘kuwatonya’ ili wajiandae.
Aidha, alisema walimtuhumu kuwa kutokuwatonya kumekidhalilisha chama na kukiweka kundi moja na CCM, hivyo anastahili kuadhibiwa vikali kwa kuwa katika taarifa yake alikuwa na nia mbaya na chama.
“Napenda kusisitiza kwamba hakuna chama ambacho kimewahi kukaguliwa na CAG, natambua kwamba mahesabu ya chama changu yamekaguliwa na wakaguzi wa nje kwa utaratibu tuliojiwekea, lakini matakwa ya kisheria ni kwamba mahesabu ya vyama vya siasa hayajakaguliwa na CAG, hili ni kosa la kisheria, bila kujali kosa limetendwa na nani,” alisema Zitto.
KIGOMA WATULIZWA
Katika hatua nyingine, Katibu Chadema Mkoa wa Kigoma, Msafiri Wamalwa, amewataka wanachama kuacha mara moja tabia ya kuchana bendera na kadi na atakayebaininka hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi yake.
Wamalwa alisema kitendo walichokifanya wanachama hao cha kuchana bendera na kadi za chama hicho kwa madai kuwa Zitto amevuliwa vyeo vya chama hicho, hakikubaliki.
Aidha, alisema Chadema Mkoa wa Kigoma kinapinga kitendo cha baaadhi ya watu wanaojiita wanachama wa chama hicho kuharibu mali za chama na kwamba ni kitendo cha jinai.
“Atakaye kamatwa atakabiliwa na mshitaka ya jinai, hivyo wanachama wasije wakafikiria chama kimekaa kimya dhidi ya kitendo walichofanya cha kuchana bendera na kuzifunga kwenye magari na kuziburuza barabarani. Ni kitendo kisichofurahisha na kisicho cha ustaarabu,” alisema.
Alisema kuwa jana uongozi wa chama hicho uliitwa kwa na Mkuu wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai Mkoa wa Kigoma, Dismas Kisusi, na kuuzwa kibali cha maandamano yaliyofanyika juzi walipata wapi.
Alisema viongozi wa Chadema walijibu kuwa hawajui kama kulikuwa na mandamano.Alisema viongozi wa Chadema waliwaomba polisi wasiwakamate wanachama hao ili kuepusha vurugu zaidi, hivyo wakiachie chama kiwakemee na kuwapa nasaha waliofanya vurugu hizo.
“Sisi kama Mkoa hatuna maamuzi wala ubishi wa kauli na maamuzi ya kikao cha juu, kwa hiyo sisi tunaheshimu maamuzi yaliyofanyika.Sisi tunafuata utaratibu wa kudumisha amani na kuwaweka wanachama sawa,” alifafanua.
Kamanda Kisusi alipo ulizwa na kuhusiana na tukio hilo, alisema hakuna mtu anayeshikiliwa na polisi kwa sababu chama hakikwenda kulalamika. Imeandikwa na Salome Kitomari, Dar na Joctan Ngelly, Kigoma.
CHANZO: NIPASHE
No comments:
Post a Comment