Baadhi
ya Ng’ombe sita mali ya John Theodore Ghumpi wa kijiji cha Minyinga
jimbo la Singida mashariki,waliokatwa katwa juzi na diwani wa CHADEMA
kata ya Mungaa Matheo Alex kwa kile kilichodaiwa kuwa ni ugomvi wa kugombea ekari 50 za mbuga.
Mkulima
na mfugaji wa kijiji cha Minyinga kata ya Mungaa jimbo la Singida
Mashariki, John Theodore Ghumpi akionyesha Ng’ombe wake aliyekatwa kwa
shoka na diwani wa kata ya Mungaa Matheo Alex kwa tuhuma ya kugombea
mbuga ya ekari 50.
Kaimu
OCD wilaya ya Ikungi, Deo Batete akiangalia kwa masikitiko Ng’ombe wa
John Theodore Ghumpi aliyekatwa shoka na diwani wa kata ya Mungaa.Wa
pili kushoto ni mkuu wa kituo kidogo cha polisi kata ya Mungaa D/S/SGT
Elibariki Urio.
Sehemu
ya shamba la Alizeti mali ya mkulima John Theodore Ghumpi mkazi wa
kijiji cha Minyinga linalodaiwa kufyekwa na diwani Matheo Alex.
Baadhi
ya wakazi wa kijiji cha Minyinga kata ya Mungaa waliofika nyumbani kwa
John Theodore Ghumpi ambaye Ng’ombe wake sita wanadaiwa kukatwa katwa
kwa shoka na diwani Matheo Alex na vijana wake wawili .Pia diwani Matheo
anadaiwa kufyeka shamba la Alizeti la ekari mbili na nusu.(Picha na
Nathaniel Limu).
Na Nathaniel Limu
DIWANI
wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kata ya Mungaa jimbo la
Singida Mashariki, Matheo Alex amewaacha midomo wazi wapiga kura wake
na wananchi wa kata hiyo kwa kitendo chake cha kukata kata ng’ombe sita
kwa shoka na kufyeka ekari mbili na nusu za shamba la Alizeti .
Imedaiwa kuwa diwani huyo kijana ametenda kitendo hicho ,kutokana na ugomvi wa kugombea mbuga ya ukumbwa wa ekari 50.
Ng’ombe
hao waliokatwa katwa na diwani Matheo akishirikiana na watoto wake,
watatu wana mimba, wawili wananyonyesha na moja ni dume wote ni mali ya
John Theodore Ghumpi mkazi wa kijiji cha Minyinga kata ya Mungaa.
Ng’ombe hao na ekari la shamba la Alizeti lililofyekwa vyote vina
thamani ya zaidi ya shilingi 4.5 milioni.
Tukio hilo la kusikitisha, limetokea mei 13 mwaka huu saa 5.00 asubuhi katika kijiji cha Minyinga jimbo la Singida Mashariki.
Diwani
Matheo ambaye miaka miwili iliyopita aliwahi kushitakiwa katika
mahakama ya hakimu mkazi mjini Singida kwa kosa la kuvunja/kuharibu kwa
makusudi kizuizi (geti) la kudhibti ushuru wa mazao ya misitu na
kumpiga mlinzi wa geti hilo,anatuhumiwa pia kufyeka ekari mbili na nusu
za shamba la Alizeti.
Akisimulia
mkasa huo wa kusikitisha, Joseph Albino (mtoto wa kaka yake mkubwa na
John mwenye ng’ombe zilizokatwa) amesema siku ya tukio alipita jirani na
kaya ya diwani Matheo na kukuta diwani akiwa kwenye kikao na watu
wasiopungua kumi.
Akifafanua,
Albino amesema alipoonwa na diwani, diwani huyo aliwaamrisha waliokuwa
kwenye kikao hicho,kuwa waanze kumuuwa yeye (Albino).
“Ghafla
diwani Matheo na kundi lake walinyanyuka huku wakiwa wamebeba shoka,
panga na hengo na kuanza kunifukuza,wakati wakiendelea kunifukuza njiani
walikuta kundi la ng’ombe za John zikichungwa na ndipo walipoanza
kuzikata kata wakiongozwa na diwani wetu”, amesema kwa masikitiko
makubwa.
Naye
mke wake John, Mary John amesema aliposikia Albino akipiga yowe, haraka
alikimbilia katika eneo la tukio na kukuta diwani akiendelea kukata
kata Ng’ombe wao bila huruma.
“Huku
nikipiga yowe, nilimwomba diwani Matheo aache kuwakata ng’ombe na
badala yake wamkate yeye hadi afe kwa madai kuwa wanakata Ng’ombe ambao
hawana hatia yoyote. Bahati nzuri waliacha zoezi la kukata Ng’ombe
wetu”,amesema kwa uchungu mkubwa.
Kwa
upande wake mwenye mali hizo shamba la Alizeti na Ng’ombe, John
Theodore Ghumpi amesema siku ya tukio hakuwepo nyumbani alikuwa Singida
mjini kikazi.
Amesema alipigiwa simu na kuelezwa juu ya tukio hilo mbaya na hivyo alirudi haraka nyumbani kwake katika kijiji cha Minyinga.
John
alisema anahisi diwani Matheo amefanya kitendo hicho kwa makusudi
kutokana na ugomvi wao wa kugombe mbuga yenye ukumbwa wa ekari 50.
No comments:
Post a Comment