Sunday, May 12, 2013

MATOKEO YA FORM 6 HAYOTATOKA MPAKA MATOKEO MAPYA YA FORM 4 YATANGAZWE:: MULUGO

 Matokeo ya mtihani wa kidato cha sita yaliyotarajiwa kutangazwa mwezi  huu yatachelewa  ili kutoa nafasi kwa Baraza la Mitihani la Taifa (Necta),  kurekebisha matokeo mabaya ya mitihani  kidato cha nne ya mwaka jana yaliyofutwa na serikali  mwezi huu.
Matokeo ya kidato cha sita ambayo huwa yanatangazwa mwanzoni  mwa mwezi Mei mpaka sasa hayajatolewa  na kwamba hayatatangazwa mpaka matokeo mapya ya kidato cha nne yatakaporekebishwa rasmi.

Alipoulizwa  juu ya suala hilo, Naibu Waziri   wa Elimu na  Mfunzo ya Ufundi  Philipo Mulugo alisema ingawa wakati huu ndio unaopaswa yatangazwe matokeo ya kidato cha sita haitafanyika hivyo hadi yatangazwe matokeo mapya ya kidato cha nne baada ya kufutwa.
http://www.ippmedia.com/media/picture/large/Philipo%20Mulugo.jpg

Hata hivyo, akasema huenda yakatolewa  pamoja au yakafuata wakati mwingine lakini mara baada ya  kukamilisha kazi ya kurejea na kusahihisha matokeo ya kidato cha nne.


"Siyo kwamba yamechelewa kwani muda wa kujiunga na chuo ni Septemba hivyo haitawaathiri kwa hilo," alisema Mulugo.


Kuhusu hatma ya wanafunzi wa kidato cha nne ambao wapo mashuleni wanaendelea na masomo ya kidato cha sita, alisema  kama kutakuwa na wanafunzi ambao wapo madarasani  shule zilizowasajili  zitakuwa hazijafuata mfumo wa elimu unavyoelekeza.


Alifafanua kuwa mfumo wa elimu kwa kidato cha nne ulibadilishwa na kwamba endapo mwanafunzi akifaulu anatakiwa kujiunga rasmi kidato cha sita  Julai na si vinginevyo.


Alisema licha ya  ucheleweshaji  wa matokeo  hali hiyo haikuwaathiri wanafunzi hao kwa kuwa ratiba ya kwenda masomoni  haijaanza kwa mujibu wa kalenda  ya shule ya serikali.


Serikali ilifuta matokeo ya kidato cha nne ya 2012 na kuiagiza Necta kuyaandaa upya kwa kutumia utaratibu wa usahihishaji na upangaji madaraja uliotumiwa mwaka  2011


Taarifa ilisema mfumo uliotumika  mwaka jana na kusababisha wanafunzi kushindwa vibaya haukufanyiwa utafiti na maandalizi ya kutosha kabla ya kutumika. 


Matokeo hayo  yaliyotangazwa  mwezi  Februari mwaka huu yalionyesha kuwa asilimia 60 ya wanafunzi walishindwa mtihani.

No comments:

Post a Comment