Tuesday, April 16, 2013

Mbio za Boston Marathon zashambuliwa kwa mabomu

Mpaka sasa watu watatu wameshakufa kutokana na mashambulio ya mabomu mawili yaliyoripuka wakati wa mbio ndefu za marathon katika mji wa Boston nchini Marekani
Mabomu mawili yaliripuka kwenye mitaa iliyokuwa imejaa watu karibu na sehemu ya kumalizia mbio za marathon. Watu wasiopungua watatu wamekufa kutokana na miripuko ya mabomu hayo yaliyoutikisa mji wa Boston katika jimbo la Marekani la Massachusettes.
Jee ni magaidi tena?

Miripuko yatikisa mji wa Boston kwenye mbio za marathoni

Watu wengine zaidi ya140 walijeruhiwa katika kadhia ya umwagikaji wa damu. Vioo vilivunjika na sehemu za miili ya binadamu ilitapakaa- hali iliyosababisha wasiwasi kwamba magaidi wameishambulia tena Marekani. Msemaji wa Ikulu ya Marekani ambae hakutaka kutajwa kwa sababu uchunguzi bado unaendelea, ameeleza kuwa mashambulio hayo yanazingatiwa kuwa ni kazi ya magaidi.
Akitoa tamko juu ya mashambulio hayo Rais Obama aliepuka kutumia neno gaidi, alieleza kwamba maafisa wa Marekani hawajui ni nani aliyeyatega mabomu hayo na kwa nini. Hata hivyo afisa mmoja wa Ikulu ya Marekani alisema baadae kuwa miripuko hiyo iliyotokea kwenye mbio za marathoni zenye jadi ya miaka mingi, inazingatiwa kuwa kitendo cha ugaidi.
Obama asema aliefanya mashambulio atapatikana:
Rais Obama alilihutubia taifa kwa kuwahakikishia Wamarekani kwamba, tukio hilo litachunguzwa kwa undani. Obama alisema "Tutabainisha nani ameyafanya mashambulio haya na kwa sababu gani." Ameeleza kuwa wote wale waliohusika, au kikundi chochote- kitauona mkono mkali wa sheria. Rais Obama amesema Marekani itamjua alieyafanya mashambulio hayo.
Mabomu hayo mawili yalipishana kwa muda wa sekunde chache tu. Mwokoaji anaetoa huduma ya kwanza, amesema wanajaribu kupata damu kwa haraka. Amearifu kuwa wapo waliojeruhiwa kwa kukatika viungo vya mwili na, wengine waliumizwa na vipande vya vioo, na pote palisambaa damu.

Maoni ya Rais Obama kuhusiana na mashambulizi

Kutokana na hali hiyo ilibainika wazi kuwa shambulio la kigaidi limefanyika muda mfupi baadae polisi waliyagundua mabomu mengine mawili ambayo yalikuwa bado hayaripuka.
Mamia ya watu walikuwa wamejipanga barabarani kushuhudia hatua za mwisho za mbio maarufu za marathon zinazofanyika katika mji wa Boston kila mwaka.
Wakimbijaji karibu alfu 23 walikuwa wanashiriki katika mbio hizo na mara tu, walisikia miripuko mikubwa miwili na waliona moshi mkubwa na vipande vya vioo - watu wote waliwambwa na kiherehere
Mtoto pia afariki
Kwa mujibu wa taarifa za polisi mtoto aliekuwa na umri wa miaka minane alikuwa miongoni mwa waliokufa. Wahudumu wa hospitali wamearifu kwamba watu 144 walijeruhiwa 17 miongoni mwao vibaya sana.
Habari zaidi zinasema ,kilometa chache kutoka kwenye sehemu ya kumalizia mbio za marathoni, pana maktaba inayoitwa "JF. Kennedy" iliyowaka moto. Lakini kamishna wa polisi ya Boston amesema mkasa huo hauhusiani na mashambulio ya mabomu.
Mwandishi: Schließ,Gero
Tafsiri:Mtullya Abdu
Mhariri: Josephat Charo

No comments:

Post a Comment