Thursday, April 11, 2013

HOTUBA YA WAZIRI WA WIZARA YA AFYA NA USTAWI WA JAMII MHE: DKT.HUSSEIN ALLY HASSAN MWINYI (MB) KWENYE UZINDUZI WA BARAZA LA USAJILI WA WATAALAM WA AFYA YA MAZINGIRA NCHINI TAREHE 10/04/2013.


Kaimu Katibu Mkuu Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii,
Kaimu Mganga Mkuu wa Serikali,
Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Kinga,
Mwenyekiti wa Baraza la Usajili wa Wataalam wa Afya ya Mazingira Nchini,
Msajili Baraza la Usajili wa Watalaam wa Afya ya Mazingira Nchini,
Wasajili wa mabaraza wa Kada za Afya,
Wajumbe wa Baraza la Usajili Wataalam wa Afya ya Mazingira,
Wataalam wa Afya ya Mazingira Nchini,
Wanahabari,
Wageni Waalikwa,
Mabibi na Mabwana.

Napenda kuchukua fursa hii muhimu kuwashukuru wote  kwa kufika kwenu kushuhudia kuzinduliwa Baraza hili la Wataalam wa Afya Mazingira nchini awamu ya pili. Aidha, nawapongeza sana wajumbe wote wa Baraza lililopita kwani kutokana na ushirikiano wao katika awamu ya kwanza ya Baraza hili wameweza kujenga msingi na daraja kwa Baraza la awamu ya pili ambalo tunalizindua leo. Vilevile sitakuwa mwingi wa fadhila kama sitaishukuru sekretariati ya Baraza kwa kuweza kuratibu kazi zote za Baraza lililopita na hatimaye  leo tunapokea wajumbe wapya kuendeleza yale yaliyoanzishwa katika awamu ya kwanza. ninawashukuru wote ambao mumeitikia wito kuja kuwaunga mkono wenzetu katika tukio hili la kipekee katika historia ya kada ya afya ya mazingira nchini. Nawashukuruni sana.

Ndugu Wajumbe,
Maboresho ya sekta ya afya nchini yamekuwa yakilenga mambo mbalimbali ambayo yanasaidia kudumisha huduma bora za afya kote nchini. Miongoni mwa masuala muhimu ni kuweka msingi na taratibu za kuhakikisha watoa huduma za afya wanazingatia sheria, kanuni, miiko na maadili ili waweze kutoa huduma kwa ufanisi na ubora wa hali ya juu. Hivyo pamoja na mambo mengine Wizara imetunga Sheria ya kusimamia na kudhibiti utendaji wa  Wataalamu wa Afya ya Mazingira  ya mwaka 2007, na kutengeneza kanuni za Sheria zinazojulikanazo kwa jina la kiingereza “The Environmental Health Practitioners (General) Regulations 2011” Aidha kwa mujibu wa kanuni ya 3, 4 na 5  zinazungumzia suala la Usajili, kuorodheshwa na kuandikishwa kwa Wataalam wa Afya ya Mazingira Nchini.

Ndugu Wajumbe,
Kada ya Afya ya Mazingira ni miongoni wa Taaluma muhimu ulimwenguni hususan katika nchi yetu ambayo ipo Kusini mwa jangwa la Sahara. Nchi nyingi zinazoendelea hivi leo zinakabiliwa na changamoto na tekinolojia endelevu, vitendea kazi duni, mazingira duni yasiyoridhisha kiafya, hali mbaya ya uchumi, soko la ajira, uzembe na uzururaji, ushindani wa kitaaluma, mabadiliko ya tabianchi ‘kuongezeka kwa joto duniani’  mabadiliko katika sekta ya viwanda na biashara, sekta ya kilimo na chakula, sekta ya nishati na madini, sekta ya elimu na pia katika sekta ya afya na ustawi wa jamii. Katika sekta ya Afya na Ustawi wa jamii kuna changamoto nyingi zikiwemo za ongezeko la milipuko ya magonjwa kutokana na uchafuzi wa mazingira. Afya ya mazingira ni suala mtambuka ambalo hushughulikiwa na wadau tofauti tofauti. Ni muhimu  utekelezaji wa majukumu haya  kuwe na ushirikishaji wa sekta wadau wa afya ya mazingira ili kutoa matokeo yenye  tija na ubora wa juu. Ni matumaini yangu kuwa tutafanya kazi kwa ushirikiano mkubwa ili kupambana na changamoto nyingi zinazotukabili hasa kuzuia maambukizi ya magonjwa.

Ndugu Wajumbe,
Katika miaka ya hivi karibuni kumekuwepo kwa matukio ya ukiukwaji wa maadili katika utoaji wa huduma za afya ya mazingira nchini, ambapo matatizo ya kitaalam hutolewa maamuzi bila ya kuzingatia taratibu na misingi ya taaluma. Hili ndilo lilipelekea kuanzishwa kwa Baraza la Usajili wa Wataalam wa Afya ya Mazingira nchini kama chombo pekee cha kusimamia na kudhibiti utendaji wa maafisa  Afya Mazingira nchini. Pamoja na mambo mengine muhimu, Baraza la awamu ya kwanza limeshaweka msingi wa utaratibu namna ya kuwasajili wataalamu mbalimbali wa fani hii, kwa kutengeneza kanuni zilizoainishwa chini ya Sheria hii, kuinua hali ya nidhamu na maadili katika taaluma ya afya ya mazingira, kukuza soko la ajira la wataalamu wa kada hii ndani na nje ya mipaka ya nchi yetu, na kuwasaidia wataalamu wa afya ya mazingira kwa kuweka taratibu wezeshi katika kujiendeleza na kupanua wigo wa ufahamu wa masuala yote yanayohusu afya na usafi wa mazingira.

Ndugu Wajumbe,
Ni matarajio ya Serikali kuwa kwa kutumia  baraza hili, mambo yafuatayo yatawanufaisha wananchi;
Huduma ya afya ya jamii  hapa nchini itatolewa kwa viwango vinavyotakiwa na hivyo kuboresha maisha ya wananchi. Baraza litasimamia na kudhibiti utoaji wa huduma ya afya ya mazingira kwa misingi ya haki.
Wataalam wa kada hii watajiendeleza na kufikia kiwango cha juu cha elimu tofauti na miaka iliyopita ambapo wengi waliridhika na kubaki katika eneo moja kwa muda mrefu na kusababisha kudumaa kwa taaluma.
Kuendelea kutengeza kanuni, viwango na taratibu zitakazoweka taratibu sahihi za kiutendaji na ili kuendana na wakati.
Uwezekano mkubwa wa kupunguza ongezeko la kasi ya magonjwa. Vifo na madhara mengine katika jamii yatapungua kwa kuwa huduma ya afya ya jamii itaboreshwa. 

Sheria imeweka na kuainisha majukumu na mamlaka ya baraza kama ifuatavyo;
Kuweka bayana majukumu ya makundi ya wataalamu wote wanaostahili kusajiliwa na hivyo kutoa huduma ya afya ya mazingira hapa nchini chini ya Sheria hii.
Kuweka bayana adhabu zitakazotolewa kwa wataalamu watakaokiuka kanuni, taratibu na maadili ya kitaalamu ya wataalamu wa fani hii kwa mujibu wa Sheria.
Kusajili wataalamu wa afya ya mazingira kulingana na viwango vya utaalamu wao.
Kuweka vipengele mbalimbali vya kisheria ambavyo vitasimamia utekelezaji wa kazi za Baraza n.k
Kuainisha vyanzo vya mapato mbalimbali ya baraza kwa ajili ya uendeshaji wa shughuli zote za baraza.

Ndugu Wajumbe,
Katika kuhakikisha kuwa Baraza la kusajili wataalamu wa afya ya mazingira linafanya kazi yake ipasavyo, sheria imebainisha  muhula wa utendaji kazi Baraza teule, ambayo ni miaka mitatu kuanzia tarehe ya uteuzi. Kwa kuzingatia hili ni vema Baraza likajitahidi kufanya kazi kwa bidii ikiwezekana ifikapo mwaka 2015 kuwepo na taarifa nzuri ya utendaji  kuzidi Baraza la awamu ya kwanza .

Baada ya kusema hayo machache niwaombe wananchi kutoa ushirikiano kwa wataalamu hawa wa afya ya mazingira nchini kwa vile majukumu yao yanategemea sana na ushirikiano wenu. Aidha nawaagiza wataalamu wa afya ya mazingira nchini kufanyakazi kwa kuzingatia maadili ya kitaaluma. Naagiza pia Baraza litekeleze majukumu yake kwa kuzingatia misingi ya sheria na taaluma.

Baada ya kusema hayo napenda sasa nitamke kuwa Baraza la Usajili wa Wataalamu wa Afya ya Mazingira nchini leo tarehe 10 Aprili, 2013, limezinduliwa Rasmi.



Ahsanteni kwa kunisikiliza.

No comments:

Post a Comment