Wednesday, March 27, 2013

MATUKIO YA MIMBA KWA WANAFUNZI YAPUNGUA WILAYANI HANDENI

MATUKIO ya kuwatia mimba/kuwabaka wanafunzi yaliokuwa yameshamiri katika shule mbalimbali za msingi na sekondari wilayani Handeni sasa yameanza kupungua tofauti na ilivyokuwa awali. Kwa mujibu wa uchunguzi uliofanywa na mwandishi wa habari hizi kwa kushirikiana na Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania (TAMWA), Machi 2012 na Machi 2013 matukio ya mimba yanapungua.
Picture
Ofisa Elimu wa Wilaya ya Handeni, Mgaza Muchiwa akizungumza na mwandishi wa habari hii
Akizungumzia hali hiyo juzi Wilayani Handeni, Ofisa Elimu wa Wilaya, Mgaza Muchiwa alisema matukio ya mimba kwa wanafunzi yanapungua tofauti na miaka ya nyuma ambapo matukio ya utoro wa mimba kwa wanafunzi yalikuwa mengi.
“Picha ya mwaka jana niliiona na tulikuwa tukifuatilia kwa karibu matukio ya kesi za mimba kwa wanafunzi…huwezi kufananisha na ilivyo sasa kunamabadiliko kwani matukio haya yamepungua,” alisema Muchiwa akizungumza na mwandishi ofisini kwake Handeni juzi.  
Picture
Mkuu wa Polisi Wilaya ya Handeni, Zuber Chembera akizungumza
Mkuu wa Polisi Wilaya ya Handeni, Zuber Chembera alithibitisha pia kupungua kwa kesi za mimba zinazofikishwa katika vituo vya Polisi ukilinganisha na hapo nyuma. Akifafanua zaidi kupitia taarifa za Dawati la Jinsia na Watoto Kituo cha Handeni, alisema hadi Novemba 2012 walipokea kesi 66 za matukio hayo lakini tangu hapo hadi Machi mwaka huu kesi hizo zimepungua kwa kiasi kikubwa.

Uchunguzi uliofanywa na TheHabari.com hivi karibuni katika shule za sekondari Komnyang’anyo, Kileleni na Kivesa zote za wilayani Handeni umeonesha kupungua kwa matukio ya mimba kwa wanafunzi, huku walimu wakidai hali hiyo imechangiwa na kampeni ya ‘Niache Nisome’ iliyoanzishwa na Mkuu wa Wilaya mpya, Muhingo Rweyemamu.
Picture
Mkuu wa Wilaya ya Handeni, Muhingo Rweyemamu
“Kweli kampeni ya ‘Niache Nisome’ iliyoanzishwa na Mkuu wa Wilaya mpya imesaidia sana maana watu wameanza kuogopa kuwarubuni wanafunzi…hata wazazi na wanafunzi nao wanaogopa kuhusishwa katika kesi hizo hii imesaidia kupunguza matukio ya mimba,” alisema Kaimu Mkuu wa Shule ya Sekondari Komnyang’anyo Nadhiru Kinyama.

Mkuu wa Wilaya hiyo, Rweyemamu Agosti 2012 alianzisha kampeni ya kupambana na watu waliyokuwa wakiwakatisha masomo wanafunzi kwa kuwatia mimba na kuwaozesha kwa kuwachukulia hatua kwa mujibu wa sheria, ikiwa ni pamoja na kutoa elimu kwa wanafunzi na jamii juu ya umuhimu wa elimu wilayani humo.

---
Habari hii imeandaliwa na timu ya THEHABARI.COM kwa ushirikiano na  TAMWA

No comments:

Post a Comment