Hakuishia hapo aliwafuata pale walipoamrishwa kukaa akawa anamchomoa anaemtaka na kumpa kipigovile alivyojiskia ili amalizie hasira zake. |
Kumbuka kipigo hicho kinafanyika mbele ya kituo cha polisi huku kukiwa na ulinzi mkali umeimarishwa. |
Alichagua kama maembe au mpira na kuchezea alivyotaka! |
SIKU
moja baada ya wanafunzi wa Chuo cha Usimamizi wa Fedha (IFM), kuitisha
maandamano kushinikiza ulinzi wa polisi kutokana na vitendo vya
udhalilishaji, jana walielezea jinsi wanavyofanyiwa vitendo hivyo na
wahuni.
Wanafunzi hao ambao wamepanga katika
nyumba zilizoko Kigamboni, wamedai kudhalilishwa na wahuni hao kwa
kuporwa vifaa vyao kama kompyuta, fedha na vitu vingine na hata kubakwa
na kulawitiwa.
Rais wa Serikali ya Wanafunzi IFM
(IFMSO), Michael Charles jana alieleza jinsi udhalilishaji dhidi ya
wanachuo wawili wanaume wa chuoni hapo ulivyotokea Januari 12, mwaka
huu.
“Kulikuwa na wanafunzi wanne walikuwa wakijisomea chumbani kabla ya
kuvamiwa usiku wa manane na watu wasiowatambua wapatao wanane.”
“Watu hao walikuwa wanataka kompyuta,
simu, fedha na vitu vingine na vile ambavyo hawakuwa navyo, walizua
tafrani kati yao... Hawa jamaa walikuwa kwenye nyumba yao iliyoko Uwanja
wa Machava.”
“Katika sakata hilo, wanafunzi wawili
walipata upenyo na kukimbia, lakini wawili walikosa na kuendelea
kupambana na wahuni hao ambao waliwazidi nguvu kutokana na wingi wao na
kuwaingilia kinyume na maumbile.”
“Kwa kweli ilituuma sana baada ya
kupata bahari zile. Waliwadhalilisha sana... Jamaa walipora mali za
wanafunzi hao na zaidi ni kompyuta, fedha na simu. Tumekuwa tukiripoti
matukio haya mara kwa mara polisi, lakini hakuna hatua zozote
zilizochukuliwa kwani vitendo hivi ni vya muda mrefu.”
“Kuna siku nyingine, wanafunzi
walikuwa wakijisomea usiku, mara wakavamiwa na wahuni hao na
walipotakiwa watoe kompyuta, simu na fedha na pale inapotokea hawakuwa
navyo ama kuwabishia, basi wanajeruhiwa kwa mapanga.”
“Hiyo ni kweli kabisa, dada zetu
wanabakwa sana tu ila hawasemi kwa kuogopa aibu katika jamii na hata
taarifa zinapofikishwa polisi tunaishia kupewa RB tu halafu tunaambiwa
watafuatilia.”
“Hawa watu si kwamba ni wageni,
wanafahamika na hata maeneo yao wanayofanyia uharamia huo
yanafahamika... Ukweli wanatunyima uhuru kabisa na tumesharipoti polisi
lakini hakuna kinachoendelea. Tumeporwa zaidi ya kompyuta ndogo 300,
kinachotuuma zaidi, hawa wezi wanafahamika wanapokaa na polisi
inawaangalia.”
Wanafunzi wengine
Baadhi ya wanafunzi hao wanaoishi
Kigamboni walidai kuwa wanaishi katika mazingira hatarishi kwani wakati
mwingine uporaji hufanyika kweupe saa 11 jioni.
Maeneo yaliyotajwa kuwa ni hatari na
wakazi wa Kigamboni ambayo wenyeji hulazimika kuyapita kabla ya saa
12:00 jioni ni Midizini, Minazi Mikinda, Mnara wa Rada, Kisimani na
Serengeti.
Mwanachuo mwingine ambaye aliomba
jina lake lihifadhiwe alisema: “Tofauti za kimaisha baina yetu ndiyo
zinazosababisha chuki kuwa wanachuo wanaringa na kujiona wenye hadhi za
juu ndiyo maana wanafanyiwa vitendo hivyo.
Wakazi nao wanena
Baadhi ya wakazi wa Kigamboni walisema kuwa mji huo ambao umepangwa kuwa wa kitalii sasa si salama.
Mmoja wa wakazi hao ambaye pia
aliomba jina lake lisiandikwe gazetini alisema inapofika saa moja usiku,
vitendo hivyo vya uporaji wa kutumia mapanga huanza na kuongeza kwamba
kinachowasikitisha ni Jeshi la Polisi kufumbia macho vitendo
hivyo.
Mwingine alisema wamekuwa wakipata usingizi wa shaka kutokana na
kujawa hofu kuwa muda wowote wanaweza kuvamiwa na kuporwa.
Wakazi hao walisema kutokana na
wahusika kutochukuliwa hatua, wanashawishika kuamini kuwa kuna ushirika
kati ya baadhi ya polisi na wahalifu hao.
“Wezi wote hapa tunawafahamu na
polisi pia wanawafahamu, inasikitisha kwamba wanamkamata mhalifu,
wanamfikisha kituoni na kesho anadunda mtaani kama kawaida,” alisema.
“Hali ya Kigamboni ni tete, mambo
haya yalianza kidogokidogo lakini sasa yamekithiri na polisi wanajua...
Nenda katika fukwe ambazo watu wanapumzika. Kuna uporaji na wakati
mwingine hutokea mauaji,” aliongeza mkazi mwingine.
Wakati wakazi hao wakizungumza hayo,
juzi Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Suleiman Kova
aliwataka wanafunzi hao wanapoona kuwa matatizo yao hayashughulikiwi
ngazi za chini, wayaripoti ngazi za juu.
Hata hivyo Kamanda huyo aliahidi
kushughulikia matatizo hayo mara moja na kusema kwa kuanzia, ataongoza
vijana wake kufanya msako wa wahalifu wote wanaohusika na vitendo
hivyo.
Mbunge Kigamboni akiri
Mbunge wa Kigamboni, Dk Faustin Ndungulile
alisema eneo la Kigamboni kwa sasa si salama kutokana na kukithiri kwa
vitendo hivyo vya uhalifu.
Akizungumza Dar es Salaam jana, Dk.
Ndungulile alisema uhalifu huo unachangiwa kwa kiasi kikubwa na ukosefu
wa ajira kwa vijana hasa baada ya kuzuiwa kwa shughuli za ujenzi
kutokana na Mradi wa Ujenzi wa Mji Mpya wa Kigamboni.
“Taarifa ya vitendo vya uhalifu
ninayo, baadhi ya wanafunzi walikuja kwangu kama mwezi mmoja uliopita na
kunieleza matatizo yao na nikawasiliana na Mkuu wa Kituo cha Polisi
Kigamboni, ambaye naye alinijulisha kwamba tayari wamewakamata vijana 15
wakihusishwa na vitendo hivyo.”
Mbunge huyo pia aliwataka wanafunzi
pamoja na wananchi wengine wanaoishi jimboni mwake wenye taarifa
zitakazosaidia kukamatwa kwa wahalifu zaidi wawasiliane naye mara moja.
Habari kwa hisani: www.wananchi.co.tz
No comments:
Post a Comment