Mama
Namwinji akionesha mkeka aina ya Msengele anaotandika wanapojifungulia
wajawazito wanapofika kwake
January 28th, 2013 | by Gordon Kalulunga
KATIKA vijiji vya Totowe na Mbuyuni hakuna serikali. Ni utawala
binafsi. Huku ni katika wilaya ya Chunya mkoani Mbeya.
Kwani Sera ya Afya ya mwaka 2007 inasema wajawazito kote nchini
watapata huduma bure kabla na wakati wa kujifungua. Lakini hayo hayaonekani
katika vijiji hivyo.
Pamoja na kuwepo zahanati katika kata ya Totowe, wanawake kwa
mamia wanasukumana wakitafuta kupewa huduma ya uzazi kwa wakunga wa jadi ambao
serikali haijawatambua.
Hilda Said Kawinga (80), mkazi wa kijiji cha Malangali mpoa kata
ya Totowe ni mkunga kwa miaka 30. Anaishi katika banda la vyumba viwili ambavyo
anaita sebule na chumba cha kulala.
Kwa umri wake Hilda hatetemi mikono. Kwa rekodi za sasa, ameweza
kusaidia wajawazito 70 kujifungua katika kipindi cha miezi 10 (Januari hadi
Oktoba mwaka 2012).
Kijiji cha Totowe kipo umbali upatao kilometa zaidi ya 100
kutoka Chunya mjini. Hapa ndipo wajawazito wanaita kwa jina la kirafiki,
“nyumbani salama,” kutokana na kujifungua salama na kuondoka kwa kicheko na
watoto wao mikononi.
Hapa ni nyumbani kwa Hilda. Pale kuna mafiga Ndilo jiko. Kuna
kuni. Hapa kuna vyombo vya kupikia.
Alipokaa mwandishi kuna mkeka na ndiyo sehemu inayotumika wakati
wa kusaidia wajawazito kujifungua. Wajawazito wakija, basi hakuna mgeni.
Bibi Hilda hana mkasi. Hana vyombo vya kisasa kama vya zahanati,
kituo cha afya au hospitali kwa huduma za uzazi. Hana kitanda. Hana godoro wala
mipira ambako wajawazito hujilaza wakati wa kujifungua.
Lakini hapa ndipo wanawake wanamiminika kwa huduma ya uzazi na
wanaondoka na watoto wao salama.
Akiongea kwa sauti nyembamba anasema, “Ninamworodhesha kila
anayejifungulia hapa katika daftari langu.
Nafanya hivi ili kuisaidia serikali kupata takwimu endapo
watazihitaji; ingawa tangu nimeanza shughuli hakuna kiongozi wa serikali
aliyewahi kuja kuangalia wala kuuliza kuwa ninafanyaje kazi.”
Hilda anajigamba kwamba alipata ujuzi kutoka kwa mama na
kuongeza, “…kwa watoto wangu sikuwahi kujifungulia hospitali; ilikuwa kazi ya
mama. Hapo ndipo nilijifunzia kazi tena bila vifaa vya kisasa. Sharti kuu ni
kuwa msafi tu.”
Hivi sasa anasema anapokea wajawazito 10 kwa mwezi na kila mmoja
anaondoka kwa kicheko. Tangu aanze kazi hii, hakuna mtoto wala mama aliyepoteza
maisha akiwa mbele yake.
Bibi Hilda ni kama mkunga mwingine Agripina Frederick Sikanyika
wa kijiji cha Mbuyuni wilaya ya Chunya. Tofauti ni kwamba Agripina ametenga
nyumba rasmi kwa wajawazito kulala na kujifungulia.
Agripina, mwenye umri wa miaka 37 anafahamika sana kwa jina la
“Mama Namwinji.” Anasema imemlazimu kuwaachia nyumba wajawazito wanaokwenda
kwake kwa ajili ya kusubiri kujifungua kutokana na idadi yao kuongezeka
kukicha.
Katika kipindi cha miezi 10, Januari
hadi 9 Oktoba 2012, Mama Namwinji amehudumia wajawazito 212. Alianza huduma kwa
wajawazito mwaka 2000.
Kwa Mama Namwinji, idadi ya waliojifungulia mikononi katika
kipindi hicho ni rekodi. Mwaka 2011 ni wajawazito 98 waliojifungulia kwake.
Kitu kimoja kimemkwaza Mama Namwinji.
Watoto wawili kati ya 212 waliozaliwa mwaka jana walikuwa na
ulemavu. Ilikuwa Septemba 15, 2012 wakati mwanamke mmoja alipojifungua mtoto
mwenye sikio moja, mguu mmoja, mdomo na pua vikiwa vimeungana. Mtoto huyo
alifariki muda mfupi baada ya kuzaliwa.
Siku iliyofuata, Septemba 16, 2012 alizaliwa mtoto aliyekuwa na
kichwa kikubwa chenye umbile la kichwa cha ng'ombe lakini mwenye kiwiliwili cha
binadamu.
Mkunga amesema hawezi kutoa majina ya waliojifungua “watoto wa
ajabu” kwa alichoeleza kuwa ni siri ya wazazi wao na aliyekuwepo.
Changamoto anazokabiliana nazo Agripina hazina tofauti na zile
za Bibi Hilda na wakunga wengi wa jadi nchini. Hana kitanda, hivyo huwalaza
wajawazito kwenye mkeka wa matete (maarufu kama Msengele).
“Hii ni hatari kwa sababu wanaweza kupata magonjwa hasa kipindi
cha masika,” anasema Agripina.
Kama Hilda, Agripina naye anaorodhesha wajawazito katika daftari
maalum, ingawa yeye anachukua hatua zaidi kwa kuangalia kadi za kliniki na
kuzijaza mara wanapojifungua.
Anasema pamoja na kuwepo kwa kituo cha afya jirani cha Mbuyuni
(Chang’ombe), lakini wajawazito wengi wanakimbilia kwake kwa madai kwamba
wakienda hospitalini wanaweza kufanyiwa upasuaji.
“Wapo ambao walikwenda hospitalini wakafanyiwa upasuaji, lakini
walipofika hapa katika uzazi wao mwingine wameendelea kujifungua bila
upasuaji,” anasema.
Kama ilivyo kwa Bibi Hilda, Agripina naye anasema huwa hatozi
kiwango chochote cha fedha kabla na baada ya mjazito kujifungua, ingawa wote
wanakiri kwamba akinamama au ndugu zao “…huleta chochote walichojaliwa kama
asante.”
“Wanawake wengi Tanzania wanakufa kipindi cha ujauzito au baada
ya kujifungua ndani ya siku 40. Hii ni hatari sana,” anasema Dk. Magoma akiwa
anafundisha waandishi wa habari Tanzania wanaobobea katika habari za afya ya
uzazi akiwemo mwandishi wa makala haya na kuongeza kuwa, kwa upande mwingine,
watoto wanakufa ndani ya kipindi cha miezi sita baada ya kuzaliwa huku
akibainisha kwamba asilimia 57 ya wanawake wote wanaojifungua hawahudhurii
kliniki.
Mtafiti wa Masuala ya Afya nchini, Dk. Kahabi Ganka Isangula,
anasema zaidi ya wanawake 300,000 wanafariki kila mwaka wakati wa kujifungua au
wakati wa kipindi cha ujauzito kutokana na sababu mbalimbali huku 800 kati yao
wakifa kwa “matatizo yanayoweza kuzuilika.”
Kati ya vifo hivyo, asilimia 99 hutokea katika nchi
zinazoendelea hasa vijijini kwa watu maskini ambapo wajawazito wengi hutokwa na
damu nyingi wakati wa kujifungua.
Anashauri wanawake wajifungulie katika vituo vya afya akieleza
kuwa moja ya changamoto kwa huduma za wajawazito, “ni kutoa kondo la nyuma
ambalo linahitaji utaalamu.”
Hata hivyo, Dk. Isangula hapingi matumizi ya wakunga wa jadi
katika kuhudumia wajawazito. Anasema, “…hakuna ubaya wowote kwa wanawake
kujifungulia kwa wakunga wa jadi, tatizo linakuja katika upatikanaji wa vifaa
vinavyomwezesha mkunga wa jadi kumhudumia mama mjamzito katika hali ya
usalama.”
Naye Mratibu wa Huduma za Afya ya Uzazi na Mtoto kutoka
hospitali ya mkoa wa Mbeya, Prisca Butuyuyu, anasema wanatambua kuwepo kwa
wakunga wa jadi na kwamba watoto wote wanaozaliwa huko wanawahesabu kuwa
wanazaliwa nyumbani kwa sababu hakuna mwongozo wa wizara unaowatambua wakunga
wa jadi.
Sera ya Afya ya mwaka 2007 inaagiza kwamba wajawazito wapewe
huduma bure katika sehemu zote za huduma ya afya. Je, hawa wanaojifungulia kwa
Hilda na Agripina wanapata huduma gani au huduma inayotajwa haiwahusu?
Je, kama wajawazito hawapati huduma, wakunga wanasaidiwa vipi au
wanawezeshwa vipi na serikali ili wafanye kazi yao kwa ustadi na weledi ambao
tayari umedhihirishwa kwa kuhudumia mamia kwa mamia ya wajawazito waliojifungua
salama?
Majibu kwa maswali haya yako mikononi mwa serikali.
Mwandishi wa makala haya anapatikana kwa simu 0754 440749 barua
pepe kalulunga2006@yahoo.com
|
No comments:
Post a Comment