Sunday, November 4, 2012

ZITTO ASEMA UMRI WA KUGOMBEA URAIS UWE MIAKA 35

MBUNGE wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe (CHADEMA), ametaka umri wa kugombea urais ushushwe kutoka miaka 40 hadi kufikia 35.
 

Zitto ambaye amekuwa akihusishwa na harakati za kuusaka urais mwaka 2015, huku kigezo cha umri kikitajwa kuwa kikwazo, alitoa kauli hiyo jana wakati akitoa maoni yake kwenye Tume ya Mabadiliko ya Katiba iliyofika jana mjini hapa kukusanya maoni ya wabunge.
 

Akitoa maoni yake, Zitto alisema ni ushamba kwa nchi kama Tanzania kuweka umri mkubwa kama sifa ya kugombea urais.
 

“Umri wa kugombea urais, Rwanda wenzetu wanaruhusu miaka 35, Burundi miaka 35, Kenya miaka 35, Marekani miaka 35, Afrika Kusini miaka 35…Sisi ni ushamba tu, hakuna sababu ya kuweka umri mkubwa,” alisema Zitto ambaye wakati akianza kuchangia alitania akisema kuwa itakapofika mwaka 2015 atakuwa na umri wa miaka 39.
 

Mbali na Zitto, wengine waliounga mkono hoja hiyo ni pamoja na Mbunge wa Nkasi Kaskazini, Ally Keissy (CCM), Mbunge wa Tarime, Chacha Nyambari Nyangwine (CCM), Mbunge wa Nzega, Dk. Khamis Kigwangwala (CCM), Mbunge wa Viti Maalumu, Dk. Prudenciana Kikwembe (CCM) na Mbunge wa Kasulu Vijijini, Agripina Buyogera (NCCR-Mageuzi).
 

Kwa upande wake, Keissy alipendekeza umri wa kugombea urais iwe kati ya miaka 35-40 kwani umri huo ni watu wenye nguvu.
 

“Hii nchi ni kubwa sana… ina milima na mabonde, tunataka rais ambaye ataweza kutembea nchi nzima na mabonde yake, hatutaki kusikia rais ambaye baada ya siku mbili tukasikia ameenda India, Pakistan kutibiwa,” alisema.
 

Nyangwine alipendekeza miaka 35 na kuendelea na kuongeza kuwa, hali hiyo itatoa nafasi kwa vijana kushiriki, huku Dk. Kigwangala akisema haoni sababu ya umri kuwa zaidi ya miaka 35 kwa mtu kuwa rais.
 

Zitto amekuwa akitajwa kuusaka urais 2015, huku akipigania sifa ya umri kwa mtu kuwa nafasi hiyo ipunguzwe kutoka miaka 40 kwa mujibu wa katiba ya sasa hadi 35.
 

Tayari mbunge huyo wa Kigoma Kaskazini amewahi kukaririwa mara kadhaa akisema kuwa hana mpango wa kugombea tena ubunge ifikapo mwaka 2015, badala yake anajipanga kuwania urais.
 

Mbali na hoja hiyo ya umri wa urais, nyingine ambayo ilionekana kuwagusa wabunge wengi ni ile ya Muungano.
 

Wabunge wengi hasa wa kutoka Zanzibar, walionekana kutotaka Muungano uvunjwe, badala yake walipendekeza kuwe na muundo mwingine tofauti na wa sasa.
 

Walipendekeza mifumo mitatu ya muundo wa Muungano. Muundo wa kwanza ni ule wa serikali tatu, muungano wa mkataba na tatu muungano wa kuwa na rais mmoja na mawaziri wakuu wawili; mmoja kutoka Tanzania bara na mwingine Zanzibar.
 

Wabunge waliopendekeza mfumo wa serikali tatu ni pamoja na Mbunge wa Mkanyageni, Mohamed Habib Mnyaa (CUF), ambaye alitaka pia uongozi uwe wa mkataba baada ya ule wa serikali mbili.
 

“Mfumo wa sasa umeleta matatizo sana, mimi napendekeza iwepo Serikali ya Bara ambayo sijui mtaamua kuiita Mzizima au lolote na ile ya Zanzibar, na Rais wa Muungano achaguliwe na wananchi wote kulingana na mzunguko wa kubadilishana,” alisema mbunge huyo.
 

Baadhi ya wabunge waliopendekeza muundo wa serikali tatu na ule wa mkataba ni pamoja na Mbunge wa Tumbe, Rashid Ali Abdallah (CUF), Mussa Kombo (Chake Chake), na Kombo Hamis Kombo (Magogoni) ambao wote ni wabunge wa CUF.
Wengine ni wabunge wa viti maalumu, Easter Bulaya na Diana Chilolo, wote kutoka CCM.
 

Kwa upande wa wabunge waliokuwa wakiunga mkono mfumo wa serikali mbili, wengi wao walionekana kuwa ni wa CCM.
Miongoni mwao ni pamoja na Mbunge wa Manyoni Mashariki John Chiligati (CCM), Mbunge wa Bunda, Steven Wassira (CCM), Mbunge wa Dole, Silvester Mabumba (CCM), Mbunge wa kuteuliwa na Rais, Zakhia Meghji, Mbunge wa Iramba, Mwigulu Nchemba (CCM) na wengine. Hata hivyo, wabunge hao waliokuwa wakitetea muundo wa serikali mbili walipendekeza uwepo utaratibu wa kushughulikia kero zinazowakabili Wazanzibari, huku wakitaka iundwe tume ya kushughulikia kero hizo.
 

Wengine walipendekeza Zanzibar iachwe huru katika masuala ya mafuta, bandari pamoja na kutaka isaidiwe kiuchumi.
 

Katika hilo, Chilligati alisema; “Kama muungano ungekuwa ni sumu inayojaribiwa, tungethubutu kuuvunja kwa muda kidogo, kule Zanzibar Watanzania elfu 15, na Wanzanzibari walioko bara laki 2.5 waonje adha ya kutafuta hati ya kusafiria au waambiwe wahame, tungejaribu kufanya hivyo.”
 

Alikosoa mfumo wa serikali tatu, Chiligati alisema unaongeza gharama kwa sababu utahitaji Baraza la Mawaziri na rais mwingine, na kwamba Tanganyika iliyokufa itabidi ifufuliwe.
 

Mbali na hilo, suala la mgombea binafsi nalo lilichukua nafasi kubwa katika maoni waliyokuwa wakichangia wabunge hao.
Wabunge wengi walipendekeza Katiba ijayo itamke wazi juu ya mgombea binafsi, ikiwa ni pamoja na uwepo wa Mahakama ya Katiba.
 

Aidha, wabunge wengi walitaka viti maalumu viondolewe na kupendekeza mfumo mwingine wa kuwanyanyua wanawake, ikiwa ni pamoja ule wa kutaka mbunge anayesimama katika jimbo asimame na mgombea mwenza mwanamke na atakapopita, mgombea mwenza naye atakuwa mbunge.
 

Suala la ukubwa wa madaraka ya rais nalo lilionekana kuwagusa wabunge wengi, ambao karibu wote waliochangia wakiwamo wachache wa CCM, walitaka yapunguzwe.
 

Pia walitaka utaratibu wa mawaziri kutokana na wabunge, ufutwe na kupendekeza mawaziri wateuliwe nje ya Bunge na wawe wataalamu wa wizara husika.
 

Kuhusu suala la mihimili mitatu, yaani Serikali, Bunge na Mahakama, wabunge wengi waliotoa maoni walitaka Katiba ijayo itamke wazi kuwa ni kosa kuingiliana na mihimili mingine.
Kwa upande wa wahujumu uchumi, baadhi ya wabunge waliotoa maoni walitaka watakaobainika kujihusisha na vitendo hivyo wanyongwe.
 

Mbunge wa Kasulu Mjini, Moses Machali (NCCR-Mageuzi), alisema hakuna sababu ya kulinda haki ya mhujumu uchumi ambaye amepewa mabilioni ya fedha kwa ajili ya kununulia dawa na badala yake anaweka fedha mfukoni halafu unalinda haki ya mtu mmoja.
 

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Tume ya Katiba, Jaji Joseph Warioba, ambaye alipata wakati mgumu, alisema kabla ya kuanza kukusanya maoni kwa wabunge alipata woga.