Gedius Rwiza
SIKU moja baada ya Mnadhimu wa Kambi ya Upinzani Bungeni, Tundu Lissu
kusema atawasilisha hoja ya kumshtaki Rais Jakaya Kikwete iwapo
atashindwa kuwaondoa kazini majaji wasio na sifa aliowateua, Ikulu
imemwambia aendelee na mchakato wake.
Mkurugenzi wa Mawasiliano Ikulu, Salva Rweyemamu alisema jana kuwa
hakuna anayemzuia Lissu kushtaki kama anaona kuna sababu za kufanya
hivyo.“Lissu ni Mbunge na ana haki zake za msingi na kama amefikia hatua
hiyo anaweza kufanya hivyo...hakuna mtu ambaye anaweza kumkataza. Nani
mwenye uwezo wa kuingilia uhuru wa mtu?”
Akizungumza na waandishi wa habari katikaOfisi za Bunge jana, Lissu
alisema amechukua uamuzi huo baada ya kuona Bunge limeikalia ripoti ya
Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge iliyomhoji kuhusu kauli
yake ya kuwatuhumu majaji kuwa baadhi yao hawana sifa.
Alisema ameamua kuchukua hatua hiyo baada ya kuona Rais Kikwete ambaye
ana mamlaka ya kuteua majaji, ameshindwa kuwaondoa kazini majaji hao
wasiokuwa na sifa.
Lissu alisema atawasilisha hoja yake hiyo kwa kutumia Kanuni ya Bunge
sehemu ya 11,Ibara ya 121, 122, 123, 124, 125 na 126 na pia kwa kutumia
Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Ibara ya 146 A.
Sehemu ya 11 ya Kanuni ya Bunge, Ibara ya 121 inaeleza kuwa mbunge
yeyote anaweza kuwasilisha kwa Spika taarifa ya hoja ya kumshtaki Rais
kwa madhumuni ya kumuondoa Rais madarakani kupitia azimio la Bunge kwa
mujibu wa Ibara ya 46 A ya Katiba ikiwa inadaiwa kwamba Rais; ametenda
vitendo ambavyo kwa ujumla vinavunja katiba au sheria ya maadili ya
viongozi wa umma.
Lissu alisema atakusanya saini za wabunge kuunga mkono hoja yake ambayo
ni asilimia 20 kwa mujibu wa Kanuni za Bunge. Wabunge wote kikatiba ni
357.
Julai 13, mwaka huu wakati akitoa maoni ya kambi ya upinzani katika
Wizara ya Katiba na Sheria bungeni, Lissu alisema uteuzi wa majaji
umegubikwa na ukiukwaji wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano.
Alisema baadhi ya majaji walioteuliwa hawana sifa, uwezo na kwamba hawakufaa kufanya kazi hiyo.
Kauli hiyo ilisababisha Bunge kuiagiza Kamatiya Haki, Maadili na
Madaraka ya Bunge inayoongozwa na Mbunge wa Mlalo (CCM), Hassan Ngwilizi
kumhoji ili athibitishe kauli yake.
Alisema wakati akihojiwa na kamati hiyo, pamoja na nyaraka nyingine,
aliwasilisha nakala ya ripoti ya kikosi kazi kilichoundwa mwaka 2008 na
aliyekuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Johnson Mwanyika na aliyekuwa
Katibu Mkuu Kiongozi, Philemon Luhanjo kuchunguza uteuzi wa majaji
nchini.
Alisema ripoti ya kikosi kazi hicho kilibaini kuwapo majaji ambao hawana
sifa ya kufanya kazi hiyo, lakini Rais Kikwete ameshindwa kuwaondoa
kazini.
Lissu ambaye pia ni Mbunge wa Singida Mashariki kwa tiketi ya Chadema,
alisema haliya Mahakama ni mbaya, kwani kuna majaji wawili ambao
waliwahi kukamatwa kwa rushwa wakiwa mawakili, lakini wakateuliwakufanya
kazi hiyo.
Alisema baadhi ya majaji hawana uwezo hata wa kuandika hukumu kutokana
na kutojua vyema lugha ya Kiingereza ambayo ndiyo inayotumika katika
Mahakama Kuu na Mahakama ya Rufani.
Alisema ili mtu aweze kuchaguliwa kuwa Jaji wa Mahakama Kuu lazima awe
na elimu ya shahada ya kwanza ya sheria, awe ametumikia miaka 10
mahakamani na anayechaguliwa kuwa jaji wa Mahakama ya Rufani lazima awe
ametumikia miaka 15 mahakamani.
Mbali ya kueleza hayo, Lissu alisema kwamba alitoa pia katika kamati
hiyo, ushahidi unaoonyesha kuwa kuna jaji mmoja wa Mahakama Kuu ambaye
hawezi hata kuandika sentensi moja ya Kiingereza ilinyooka... “Kama jaji
hawezi kuandika hata sentensi moja ya Kiingereza ilinyooka, tunaweza
vipi kuwa na Mahakama inayotenda haki?”
Alisema kuna jaji mwingine ambaye ameongezewa mkataba wa kufanya kazi
mara ya tatu kitu ambacho ni kinyume cha sheria. Alisema kwa mujibu wa
Tume ya Mahakama, hakuna jaji ambaye anaweza kufanya kazi kwa mkataba
kwa vipindi vitatu.
Kama Lissu atachukua hatua hiyo, itakuwa ni mara ya pili kwa mbunge
kuwasilisha bungeni hoja ya kutaka kumwajibisha kiongozi wa juu
serikalini.
Mara ya kwanza alikuwa Mbunge wa Kigoma Kaskazini (Chadema), Zitto Kabwe
katika Bunge lililopita alipokusanya saini za wabunge kutaka kupiga
kura ya kutokuwa na imani na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda akitaka
awawajibishe baadhi ya mawaziri waliokuwa wametajwa kuhusika katika
matumizi mabaya ya madaraka katika Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa
Hesabu za Serikali (CAG).
Hata hivyo, Rais Kikwete alifanya mabadiliko makubwa katika Baraza lake la Mawaziri hivyo kuzima hoja hiyo ya Zitto
Habari hii kwa msaada wa Mtandao