Wednesday, October 31, 2012

TAMKO LA JUMUIYA YA MAIMAMU ZANZIBAR KUHUSIANA NA VURUGU ZILIZOTOKEA

KUHUSU VURUGU, FUJO, VITENDO VYA UVUNJIFU WA AMANI, KUNYANYASWA , KUDHALILISHWA NA KUPIGWA WANANCHI WASIO NA HATIA.
Sifa zote njema anastahiki Allah (S.W) Muumba wa mbingu na ardhi na vyote vilivyomo. Sala na salamu zimfikie kipenzi cha Umma Mtume Muhammad (S.A.W) jamaa zake, Maswahaba zake na wale wote wanaowafuata kwa wema hadi siku ya malipo.
Kwa mara nyengine tena nchi yetu imetumbukia katika vitendo vya vurugu, fujo, uharamia na vitendo vya uvunjifu wa amani kuanzia tarehe 17 hadi 19 Octoba 2012 kufuatia kutoweka kwa Sheikh Farid Hadi katika mazingira ya kutatanisha. Vikundi vya Maharamia kwa kutumia kichaka cha kutekwa “Sheikh Farid Hadi” walitekeleza hujuma kubwa sana ambayo imepelekea maafa kadhaa ikiwemo kumwaga damu za watu, kuharibiwa mali za watu, kutia khofu kubwa wananchi, kuashiria kusambaratika kwa Umoja, kuvunja heshima za watu, na kuharibiwa kwa miundo mbinu.
JUMAZA kama ilivyotangulia kusema kufuatia vurugu na fujo katika uchaguzi mdogo wa Bububu, kuwa kipo kikundi cha watu wanaotekeleza mipango yao ya kuihujumu Zanzibar kwa kupinga Serikali ya Umoja wa Kitaifa ( SUK ) ili kuwarejesha Wazanzibari katika maisha ya hasama na uadui baina yao pamoja na kupinga harakati za kupigania hadhi ya Zanzibar ndani na nje, Kimataifa. Kutokana na tatizo hili linaloendelea kukua na katika kuiangamiza Zanzibar, JUMAZA inatoa tamko lifuatalo:-

  1. JUMAZA inawatanabahisha wananchi wote kuwa Taasisi za kiislamu Zanzibar kamwe hazihusiani na vurugu hizo kwani zenyewe zinapigania amani, utulivu mshikamano umoja na udugu kama inavyoelekezwa katika Dini yetu tukufu ya Kiislamu.
  2. JUMAZA inalaani vikali wale wote waliofanya fujo na hujuma zilizopelekea maafa katika nchi yetu kwa kutumia kichaka cha “ Kutekwa Sheikh Farid Hadi”.
  3. JUMAZA inalaani vikali vitendo vya kiharamia vilivyofanywa na makundi ya kiharamia vikiwemo vya ubaya ubaya na vinginevyo. Hivyo Serikali ipambane na makundi haya yaliyomo katika jamii na kuyafuta kabisa.
  4. JUMAZA inaiomba Serikali kuunda Tume Huru ya kuchunguza kadhia ya kutekwa Sheikh Farid Hadi na ripoti yake iwasilishwe kwa uwazi kabisa kwa Wazanzibari na Jumuiya ya Kimataifa.
  5. JUMAZA inaviomba vyombo vya kisheria kuwatendea haki watuhumiwa wote wa ghasia hizo wakiwemo viongozi wakuu wa Jumuiya ya Uamsho kwa mujibu wa sheria za nchi zinavyoelekeza.
  6. JUMAZA inaviomba vikosi vya usalama viache kuwatesa na kuwadhalilisha na kuwapiga wananchi wasio na hatia bali iongeze juhudi za kuyasaka makundi ya kiharamia kwa kufuata taratibu za kiusalama na ulinzi wa nchi.
  7. JUMAZA inawaomba Wazanzibari wote kuwa watulivu na subra ya hali ya juu katika kipindi hiki kigumu ili kuepusha Zanzibar yetu tunayoipenda kutumbukia katika mapigano ya wenyewe kwa wenyewe na hivyo kuiangamiza kabisa.
  8. JUMAZA inawanasihi viongozi wetu wakuu wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa kutumia busara zaidi katika kutatua matatizo yaliyopo katika jamii yetu na kurudisha amani badala ya kuweka mbele matumizi ya nguvu.
  9. JUMAZA inawaomba Wazanzibar wote wasikubali kurejeshwa walikotoka pia wasiondoke katika ajenda yao ya kudai hadhi ya Zanzibar ndani na Kimataifa kwa njia ya amani na ustarabu na wajitokeze kwa wingi katika kutoa maoni bila ya woga wala khofu hivi sasa katika Mikoa ya Kaskazini Unguja na Pemba na baadae Mkoa wa Mjini Magharibi.
  10. JUMAZA inawataka maimamu wa misikiti kuleta dua kwa wingi kwa wiki moja na kisomo maalum (kunuti) siku ya Ijumaa kuiombea kheri, amani, mshikamano na utulivu wa nchi yetu. 
MOLA WETU MTUKUFU
TUNAKUOMBA UINUSURU ZANZIBAR NA WATU WAKE
DHIDI YA MAADUI WA NDANI NA NJE WASIOTUTAKIA MEMA- AMIN

ALI ABDALLA SHAMTE
NAIBU AMIR
JUMAZA
Chanzo: ZanzibariYetu