Friday, October 19, 2012

HALI SIYO NZURI KATIKA JIJI LA DAR ES SALAAM LEO

Askari wakiwa katikati ya jiji maeneo ya Kariakoo wakihakikisha kuwa hamna vikundi vyovyote vya waislamu vilivyokaa.


Baadae walikuja JWTZ kuongeza nguvu angalau Tafrani ilipungua

Hiki ni baadhi ya vipeperushi vilivyotolewa na waislamu hao
Hali ni tete katika Jiji la Dar es Salaam ambapo mabomu ya machozi yamekuwa yakirindima mchana huu wakati Jeshi la Polisi nchini likikabiliana na wafuasi wa dini ya Kiislamu ambao wamekuwa wakifanya maandamano makubwa sehemu mbalimbali leo.

Katika maeneo ya Kariakoo, askari wa Kikosi cha Kuzuia Ghasia (FFU) walilazimika kuendelea kutumia mabomu ya machozi kuwatawanya waandamanaji hao ambao haijafahamika mara moja lengo lao la kufanya hivyo. Watu kadhaa wamekamatwa na kufikishwa kwenye kituo cha Msimbazi.

Katika Barabara ya Azikiwe eneo la Posta Mpya hali ilikuwa tulivu huku mtaa huo ukiwa hauna watu kabisa zaidi ya askari wa FFU tofauti na ilivyozoeleka hasa katika nyakati za jioni ambapo mamia ya watu huwa wanasubiria usafiri hapo.

Maeneo ya Kinondoni nako walionekana askari wa FFU wakiwa wametanda barabarani hasa katika Barabara ya Kawawa kudhibiti hali ya usalama maeneo hayo ambapo jirani kuna msikiti mkubwa.

Imeelezwa kwamba barabara kadhaa za maeneo ya Posta na Kariakoo zimefungwa kwa muda kupisha zoezi ya ulinzi wa amani linalofanywa na vikosi hivyo vya kuzuia ghasia.

Maandamano hayo ambayo yamezaa vuguru ambazo zinaendelea hadi sasa yanahusishwa na kukamatwa na mwanaharakati wa dini ya Kiislamu, Shekhe Ponda Issa Ponda na wenzake 46 waliokamatwa na kufikishwa mahakamani juzi kwa tuhuma za uchochezi na wizi.