Frank Sanga na Anthony Kayanda, Mwananchi, Kigoma -- MBUNGE
wa Kigoma Kaskazini (CHADEMA), Zitto Kabwe amesema hana mpango wa
kugombea ubunge mwaka 2015 badala yake anajipanga kuwania urais.
Zitto
alisema hayo jana alipozungumza na wananchi katika mjadala ulioandaliwa
na asasi ya kiraia ya Meza ya Duara uliokuwa unafanyika maeneo ya Soko
la Mwanga, mjini Kigoma.
Zaidi ya watu 200, ambao walihudhuria
katika mjadala huo wa wazi walimuuliza maswali mbalimbali mbunge huyo,
huku mmoja akigusia kuhusu tetesi za mara kwamba Zitto anataka kugombea
urais katika uchaguzi ujao, “Nimefanya kazi kubwa katika kazi yangu ya
ubunge, nimeleta mabadiliko mengi kuanzia bungeni mpaka jimboni.
Nadhani inatosha na hata nikiongezewa miaka mingine sitaweza kufanya
yale yaliyonishinda katika kipindi cha miaka kumi. Kama Mungu ataniweka
mpaka mwaka 2015, sitagombea ubunge tena kwa sababu kazi niliyofanya
inatosha. Natangaza rasmi kuwa nitagombea urais kupitia chama changu cha
CHADEMA, bila kusababisha msuguano wowote na sitaki kuingia katika
historia ya kurudisha nyuma harakati za upinzani kushika dola,” alisema
Zitto.
“Nataka kuleta changamoto mpya, nitawaeleza watu wa chama
changu nia hiyo na nitatoa hoja za msingi. Hata kama sitapata ridhaa
yao, lakini huo ndio msimamo wangu. Iwapo chama kikiona sistahili au
sifai, nitakubaliana na uamuzi huo. Watu wengi wanadhani urais ni cheo,
hawajui kuwa ni nafasi ambayo inakufanya ufanye vitu ambavyo ni vikubwa
na vya maendeleo kwa wananchi.”
Katika hatua nyingine Zitto alisema ana mpango wa kuwania urais kupitia CHADEMA katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015.
“Kwanza
nataka niwahakikishia watu wa Kigoma msiwe wanyonge…mna uwezo wa kutoa
rais wa nchi hii,” Zitto alianza kujibu swali hilo.
Hata hivyo
Zitto alipoulizwa baadaye na gazeti la Mwananchi kuwa mwaka 2015 atakuwa
na miaka 39, hivyo kukosa sifa ya kugombea urais kwa mujibu wa katiba
alijibu; “Nadhani nina uwezo wa kuwa rais, sidhani kama Katiba inaweza
kumzuia mtu mwenye uwezo asigombee na ndio maana ninaamini kuwa
kipengele cha kuwa na miaka 40 kitabadilishwa katika katiba mpya.” “Nchi
za Kidemokrasia lazima vyama vibadilishane utawala wa kuongoza nchi
kama ilivyo katika nchi za Ghana na Zambia. Tanzania inatakiwa kuiga
mfano wa nchi hizo,” alisema Zitto.
Katika kukazia hilo, Zitto
alisema anashangazwa na umaskini uliopo Tanzania wakati mwaka 1976
uchumi wake ulikuwa sawa na nchi ya Malaysia, lakini mpaka kufikia mwaka
2001, Malaysia ilipunguza idadi ya watu wanaoishi chini ya dola moja
kutoka asilimia 56 mpaka kufikia asilimia tatu huku Tanzania ikipunguza
kutoka 51 mpaka 46.
Katika hatua nyingine, Zitto alikana kuwa,
Chadema ni chama cha udini, ukanda, ukabila ila akasisitiza kuwa ni
chama cha kitaifa, “Ndugu zangu naomba mnielewe, CHADEMA si chama cha
ukabila, ukanda wala udini bali ni chama cha kitaifa. Hizo ni propaganda
za wapinzani wetu,” alisema Zitto baada ya kuulizwa na mmoja wa
washiriki kuhusu tuhuma za chama hicho kuwa cha Kikanda. CCM imewahi
kudai CUF ni chama cha Waislamu, na sasa wanasema Chadema ni chama cha
Wakristo, sasa wao CCM ni chama cha wapagani au cha watu gani?” Alihoji
Zitto.
Alisema ili kuthibitisha kuwa CHADEMA si chama cha
Kikanda, matokeo ya urais wa mwaka 2010, Dkt. Wilbroad Slaa aliongoza
dhidi ya wagombea urais wengine kwa kupata kura nyingi katika Jimbo la
Manyovu mkoani Kigoma na hivyo kufanya kupata asilimia nyingi kuliko
sehemu yoyote Tanzania