Mkuu
wa ofisi na Mwakilishi wa Shirika la Kimataifa la Sayansi, Elimu na
Utamaduni (UNESCO) nchini Tanzania, Bi. Zulmira Rodrigues (kushoto)
akimpongeza Kiongozi Mkuu wa Jamii ya Kimasai Afrika Mashariki, Mokombo
Olaiboni Simeli kwenye semina ya viongozi mbalimbali wa jamii ya
kimasai, wazazi, viongozi wa shule za msingi na sekondari Wilayani
Ngorongoro, wakuu wa idara ya afya na vitengo vya ustawi wa jamii wilaya
ya Ngorongoro.
Susana
Koillah, Mama Shughuli na mtafsiri wa lugha ya Kimasai katika semina
hiyo akimsikiliza kwa makini Mkuu wa ofisi na Mwakilishi wa Shirika la
Kimataifa la Sayansi, Elimu na Utamaduni (UNESCO) nchini Tanzania, Bi.
Zulmira Rodrigues (kulia) kabla ya kutafsiri mada yake kwa wanasemina.
Sehemu
ya washiriki wa semina ya viongozi wa jamii ya kimasai, wazazi,
viongozi wa shule za msingi na sekondari, wakuu wa idara ya afya na
vitengo vya ustawi wa jamii wilayani Ngorongoro wakiwa kwenye semina
hiyo iliyofanyika Ukumbi wa Halmashauri ya Wilaya ya Ngorongoro juzi.
Afisa
mradi wa Elimu ya Afya na VVU/UKIMWI Taifa wa Shirika la Kimataifa la
Sayansi, Elimu na Utamaduni (UNESCO) nchini Tanzania, Mathias Herman
(kushoto) akitoa maelekezo kwa wana semina ya viongozi wa jamii ya
kimasai, wazazi, viongozi shule za sekondari, wakuu wa idara ya afya na
vitengo vya ustawi wa jamii wilayani Ngorongoro wakiwa kwenye semina
hiyo iliyofanyika Ukumbi wa Halmashauri ya Wilaya ya Ngorongoro juzi.
Sehemu
ya washiriki wa semina ya viongozi wa jamii ya kimasai, wazazi,
viongozi wa shule za msingi na sekondari, wakuu wa idara ya afya na
vitengo vya ustawi wa jamii wilayani Ngorongoro wakiwa kwenye semina
hiyo iliyofanyika Ukumbi wa Halmashauri ya Wilaya ya Ngorongoro juzi.
VIONGOZI
wakuu wa jamii ya Kimasai wa Afrika Mashariki wameridhia kuachana na
mila potofu zimezopitwa na wakati ikiwemo vitendo vya ukeketaji kwa
wasichana wa jamii ya kimasai ambavyo vimekuwa vikiwaathiri wasichana
hao kwa kiasi kikubwa.
Kauli
ya kusitisha vitendo hivyo ilitolewa juzi Wilayani Ngorongoro na
Kiongozi Mkuu wa Jamii ya Kimasai Afrika Mashariki, Mokombo Olaiboni
Simeli pamoja na msaidizi wake kutoka Tanzania, Sangau Naimado Olaiboni
walipokuwa katika semina ya elimu ya afya ya uzazi, kupinga vitendo vya
ukeketaji pamoja na mimba za utotoni.
Kiongozi
Mkuu wa Jamii ya Wamasai Afrika Mashariki, Olaiboni Simeli alimueleza
Mkuu wa Shirika la Kimataifa la Sayansi, Elimu na Utamaduni (UNESCO) na
Mwakilishi wa Shirika hilo Tanzania, Bi. Zulmira Rodrigues kuwa jamii
hiyo ya wamasai imeridhia kuacha mila zilizopitwa na wakati na
itaendelea kushiriki kuelimisha jamii yao zaidi juu ya madhara ya mila
hizo potofu ikiwemo ukeketaji na ndoa za utotoni.
“…Tunaishukuru
UNESCO kwa kuendelea kutoa elimu hii kwetu juu ya mila potofu nasisi
tunaungana nanyi kuendelea kutoa elimu kwa jamii yetu kupinga ukeketaji
na ndoa za utoto tumeelezwa athari nyingi zinazowapata wasichana
wanaokeketwa…kwanini tuendelee na mila zinazoleta madhara kwa watu wetu?
Tushirikiane kupiga vita hivi,” alisema Olaiboni Simeli akizungumza
mbele ya Bi. Rodrigues.
Kwa
upande wake Kiongozi Mkuu wa Jamii ya Wamasai Tanzania, Naimado
Olaiboni alisema hakuna haja ya jamii ya kimasai kuendelea na mila
zilizopitwa na wakati ilhali mila hizo zikiendelea kuwaathiri wamasai na
kuwabakiza nyuma kimaendeleo katika nyanja mbalimbali. “…Tutaendelea
kushirikiana nanyi kupinga ndoa za utotoni kwa kuwa tumeelezwa madhara
yake na wataalamu leo,” alisema Naimado Olaiboni.
Naye
Mkuu wa ofisi na Mwakilishi wa Shirika la UNESCO Tanzania, Bi.
Rodrigues alisema anapenda kuona Jamii ya Kimasai inaendeleza mila na
tamaduni zao lakini zile nzuri ambazo hazina chembe ya kiunyanyasaji kwa
makundi yote. Alisema ukeketaji kwa wasichanga unamadhara makubwa kwa
jamii hiyo hivyo haina budi mila hizo kupuuzwa ili kumlinda mtoto wa
kike na madhara yanayomkumba anapofanyiwa vitendo hivyo.
“…Napenda
kuona Wamasai wanaendeleza mila na tamaduni zao lakini ziwe nzuri na
zisizo na chembe ya ukatili wala unyanyasaji, tuangalie ni namna gani
tunaziendeleza na kubaki katika uhalisia wetu…nawahakikishia
tutashirikiana kuhakikisha hili linafanikiwa kwenu,” alisema Bi.
Rodrigues akizungumza katika semina hiyo.
Aidha
aliwashauri jamii ya Kimasai kupunguza kuwa na idadi kubwa ya watoto na
wake ilhali mume akishindwa kuihudumia familia hiyo jambo ambalo
limeendelea kuchochea umaskini wa familia hizo vijijini kwani watoto
wamekosa mahitaji ya msingi katika familia na kujikuta wakiishi kwa
taabu.
Aliwataka
Wamasai pia kupinga ndoa za utotoni kwani mabinti wadogo wanapoolewa
wanakosa fursa ya elimu pamoja na kuunda familia bora kutokana na uduni
wao katika masuala ya afya ya uzazi kiujumla na madhara yanayowaandama
katika maisha yao. “…Ndoa za utotoni nazo ni tatizo katika jamii yetu,
tuzipige vita maana mtoto mdogo anapoolewa haweza kuunda familia bora na
wala uzazi wake hauwezi kuwa bora…,” aliongeza Bi. Rodrigues.
Zaidi
ya wanasemina 210 kutoka Kata za Ololosokwani, Arash, Soit Sambu,
Oloipili, Aoliani Magaidulu wakiwemo viongozi mbalimbali wa jamii ya
kimasai, wazazi, viongozi wa shule za msingi na sekondari na wakuu wa
idara ya afya na vitengo vya ustawi wa jamii Wilayani Ngorongoro
wamenufaika na semina hiyo ya jitihada za kuelimisha jamii juu ya mila
na desturi zilizopitwa na wakati.