Florence Majani, MWANANCHI, Dar es Salaam -- BAADA
ya kimya cha muda mrefu, baba mzazi wa kiongozi wa Jumuiya ya Madaktari
Tanzania, Dkt. Stephen Ulimboka, amekubali kuzungumzia sakata la
mwanaye kutekwa, kuteswa, kutibiwa na hatimaye kurejea nchini akisema
kwamba kupona kwake ni neema za Mungu, huku akiishutumu Serikali kuwa
imewatelekeza Watanzania.
Hii
ni mara ya kwanza kwa baba huyo, Stephen Mwaitenda kuzungumza tangu
mwanaye alipotekwa, kuteswa na baadaye kutupwa katika Msitu wa Pande,
nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam.
“Naishangaa
Serikali hii ambayo wananchi wanapigwa na kuuawa bila makosa. Nakumbuka
kiongozi aliyeipenda Tanzania ni mmoja na ameshatangulia mbele za
haki,” alisema akimaanisha Baba wa taifa Mwalimu Julius Nyerere.
Mwaitenda
alitoa kauli hiyo jana baada gazeti la MWANANCHI kumtafuta ili
azungumzie habari zilizoenea nchini kwamba mwanaye, amepata kazi nje ya
nchi ambapo Mwaitenda alikanusha madai hayo akisema kuwa mtoto wake
hawezi kwenda nje ya nchi bila yeye kufahamu... “Pengine ana mipango
hiyo, lakini mimi sijui wala sijasikia, lakini atakwenda nje ya nchi
kufanya nini? Hizi habari hizo ndiyo nazisikia kwako kwa mara ya kwanza
eti Ulimboka anataka kwenda nje ya nchi? Akafanye nini alichokosa hapa
Tanzania!”
Wakati
mwandishi akiingia nyumbani kwa Mwaitenda, Ubungo Kibangu, Dar es
Salaam, alipishana na Dkt. Ulimboka akiwa kwenye gari na wenzake, wanne.
Hata hivyo, hakufanikiwa kuzungumza naye.
Kuhusu
tukio la kutekwa, kuteswa na kutupwa katika Msitu wa Pande, Mwaitenda
alisema: “Mpaka sasa, tumeiona kazi ya Mungu, ile ni neema ya Mungu kwa
sababu wewe uliona wapi mtu akapigwa namna ile halafu akapona kama si
kwa neema tu.”
Alisema
alimkanya mtoto wake huyo aachane na masuala ya migomo na siku chache
baada ya onyo lake ndipo akatekwa na kujeruhiwa vibaya, “Nilimkanya
kabisa kuhusu mambo ya migomo hasa baada ya kuniambia kuwa amechaguliwa
kuwa Msemaji Mkuu wa Madaktari wenzake na kwa bahati mbaya ndiyo
yakatokea hayo yaliyotokea,” alisema.
Alielezea
kushangazwa kwake na watu waliompiga mtoto wake akisema, hajui walikuwa
wanataka nini. Alisema hakuwa na uhasama na mtu yeyote kuanzia kazini
kwake hata kwa marafiki zake, “Mpaka sasa nashindwa kuelewa kwa nini
waliamua kumpiga, kwa sababu kwa ninavyomjua Steven, hajawahi kuwa na
ugomvi na mtu tangu anasoma shule ya msingi mpaka anamaliza chuo kikuu.
Sijawahi kupata mashtaka kuwa amegombana na mtu. Nashangaa haya
yanayotokea leo.”
Akitoa
wasifu wa mwanaye huyo alisema tangu utoto wake, Daktari huyo alikuwa
mtulivu na mwenye upeo wa hali ya juu. Alisema anasikitishwa mno na
yaliyompata akisema kwamba siku moja ukweli utawekwa wazi kwani siku
zote kazi za Mungu na kazi za shetani haziwezi kuchangamana, “Kama
mafuta na maji, ukiyachanganya... mafuta yatakuwa juu na maji yatabaki
chini. Najua siku moja Mungu ataweka wazi ukweli,” alisema.
Kuhusu
afya ya Dkt. Ulimboka, Mwaitenda alisema ingawa yeye si daktari, lakini
anamwona mtoto wake kuwa yu mwenye afya na kuongeza kuwa hata mwanaye
huyo amekuwa akisema kwamba sasa ana afya njema.
Hali nyumbani kwa Mwaitenda
Baada
ya kufika nyumbani kwa mzazi huyo wa Dkt. Ulimboka, mwandishi
alikaribishwa vyema na mzazi huyo ingawa alimtahadharisha kwamba endapo
angekutana na Daktari huyo hapo au ndugu zake, wangemfukuza, “Una bahati
ungewakuta hapa watoto wangu tusingezungumza. Hata hawa mabinti zangu
wakikukuta, hatutaendelea na mazungumzo....”
Hivyo
ndivyo ilivyotokea kwani baada ya kuelezea hayo, mabinti wake wawili
walitokea na mmoja akaanza kwa kusema... “Shikamoo Baba, umesharudi?
Huyu nani?”
Mzee
Mwaitenda, kwa bashasha aliwatambulisha mabinti hao... “Huyu ni
Florence... mwandishi wa MWANANCHI...” Hata kabla hajaendelea binti huyo
na mwenzake walimshika mkono na kumwamuru atoke nyumbani hapo mara
moja.
“Haya dada
toka, toka, mmeshindwa kuandika kuhusu mwandishi mwenzenu aliyekufa
(Daudi Mwangosi), mnakuja kutufuata mpaka huku Kibangu.... mtazame miguu
ilivyomchafuka kwa vumbi kwa kushadadia ya watu, toka kabla sijakupiga
makofi,” alisema mmoja wa mabinti hao.
Kauli ya Dkt. Mkopi, Prof. Kahamba
Rais
wa Chama cha Madaktari Tanzania (MAT), Dkt. Namala Mkopi ambaye alikuwa
karibu na Dkt. Ulimboka wakati wa mgomo wa madaktari nchini, alisema
tangu waonane aliporejea nchini kutoka Afrika Kusini, hajawasiliana
tena.
“Hatujawasiliana
naye,” alisema Dkt. Mkopi na kusema kulingana na ukubwa wa tatizo
lililompata, hakuwa na mpango wa kumsumbua, bali kumwacha apumzike hadi
atakapokuwa amejisikia mwenyewe kurejea kazini.
Aliyekuwa
kiongozi wa jopo la madaktari waliomhudumia, Profesa Joseph Kahamba
alisema, hajawahi kuonana wala kuwasiliana na Dkt. Ulimboka tangu
alipopelekwa Afrika Kusini, Juni mwaka huu.